Chanzo cha picha, Press service of the State Emergency Service of Ukraine in Odesa region
Urusi
imeongeza mashambulizi yake katika eneo la kusini mwa Ukraine la Odesa, na
kusababisha kukatika kwa umeme na kuhatarisha miundombinu ya baharini ya eneo
hilo.
Naibu Waziri
Mkuu wa Ukraine Oleksiy Kuleba alisema Moscow imefanya mashambulizi katika eneo
hilo. Wiki iliyopita, alionya kwamba mashambulizi “huenda yakaelekea Odesa”.
Rais
Volodymyr Zelensky amesema mashambulizi hayo ya mara kwa mara ni jaribio la
Moscow la kuizuia Ukraine kufanya shughuli zake kupitia bahari.
Mapema mwezi
Desemba, Rais wa Urusi Vladimir Putin alitishia kuvuruga njia za Ukraine za kuifikia
bahari kama kulipiza kisasi kwa mashambulizi ya ndege zisizo na rubani dhidi ya
meli za mafuta za magendo za Urusi katika Bahari Nyeusi.
Siku ya
Jumatatu jioni, mashambulizi yaliathiri miundombinu ya bandari huko Odesa, na
kuharibu meli ya kiraia, gavana wa mkoa alisema.
Yalikuwa ni mashambulizi
ya hivi karibuni katika mfululizo wa mamia ya mashambulizi ambayo yamevuruga
usambazaji wa umeme katika eneo hilo na kusababisha vifo
kadhaa.
Siku ya
Jumapili usiku, Mashambulizi yalikata umeme kwa watu 120,000 na kusababisha
moto katika bandari kubwa ambao uliharibu makontena mengi ya unga na mafuta.
Wiki
iliyopita, shambulio la kombora la balestiki kwenye bandari ya Pivdenniy
mashariki mwa Odesa liliwaua watu wanane na kuwajeruhi wasiopungua 30.
Shambulio
jingine mapema wiki hii lilimuua mwanamke aliyekuwa akisafiri kwa gari na
watoto wake watatu na kukata kwa muda daraja pekee la mkoa wa Odesa
linalounganisha Ukraine na Moldova.
Bandari ya
Odesa ni muhimu kwa uchumi wa nchi hiyo. Jiji hilo ni la tatu kwa ukubwa nchini
Ukraine baada ya Kyiv na Kharkiv. Sasa ni umuhimu kwani bandari zingine katika
maeneo ya Zaporizhzhia, Kherson na Mykolayiv hazifikiki kutokana na uvamizi wa
Urusi.
Licha ya
vita, Ukraine inasalia kuwa moja ya nchi zinazouza ngano na mahindi kwa wingi
duniani. Tangu Agosti 2023, Odesa imekuwa njia muhimu inayoiruhusu kusafirisha
nafaka nje ya nchi, ikifuata ufuo wa Romania na Bulgaria kabla ya kufika
Uturuki.