BEKI wa kimataifa wa Afrika Kusini, Rushine De Reuck, amekiri kuondoka kwa kocha Fadlu Davids ndani ya Simba kumempa wakati mgumu yeye na Neo Maema aliyowavuta Msimbazi.

Rushine amesema imekuwa ngumu kwake pamoja naMaema kufuatia kuondoka kwa Fadlu aliyewasilia msimu huu kabla ya kurejea Raja Casablanca.

De Reuck na Maema walijiunga na Simba mwanzoni mwa msimu huu wakati Fadlu akiwa ndiye kocha mkuu wa timu hiyo. Inaaminika usajili wa wachezaji ulifanyika baada ya mapendekezo ya moja kwa moja kutoka kwa Fadlu ambaye ni raia wa Sauzi pia.

Kuondoka kwa Fadlu kuliwashangaza mashabiki wengi wa soka nchini, akiwa ametoka kuifikisha timu hiyo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita dhidi ya RS Berkane ya Morocco.

Akizungumza na iDiski Times, De Reuck alisema tukio hilo lilikuwa gumu kwake na Maema, hasa kwa kuwa walikuwa bado wageni ndani ya timu na walitarajia kufanya kazi naye kwa muda mrefu zaidi.

“Kuondoka kwa kocha Fadlu haikuwa rahisi kwangu na Neo, hasa tukizingatia kuwa tulikuwa bado tunaingia katika timu. Tulikuwa na matumaini ya kufanya kazi naye kwa muda mrefu, lakini haikuwa hivyo. Hata hivyo, hiyo ndio soka, mambo kama haya hutokea,” amesema De Reuck.

Ameongeza, Fadlu alikuwa na mahusiano mazuri na wachezaji wote wa timu, si yeye na Maema pekee.

“Alikuwa kocha aliyekuwa na uhusiano mzuri na wachezaji wote. Kila mtu alihisi kuondoka kwake. Lakini katika soka mambo hubadilika na kilicho muhimu ni sisi wachezaji kubaki kuwa wataalamu, kumpa heshima kocha mpya, kuelewa falsafa yake, na kwa sasa mambo yanaendelea vizuri.”

De Reuck amesisitiza, Simba ni klabu kubwa yenye dhamana kubwa kwa wachezaji wa timu hiyo.

“Simba ni klabu kubwa na tuna wajibu mkubwa. Haijalishi ni kocha gani yupo madarakani, jukumu letu ni kufanya vizuri, kujituma na kuwafurahisha mashabiki wetu kama tunavyofanya kwa sasa.”

Kwa sasa Simba itakuwa chini ya Kocha Steve Barker ambaye ni raia wa Sauzi aliyetambulishwa kuchukua nafasi ya Dimitar Pantev aliyemrithi Fadlu na kukaa na timu hiyo kwa siki 61 kabla ya kutimuliwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *