SERIKALI imefanikiwa kutoa vitambulisho vya matibabu ya bure na bima za afya kwa wazee 1,256,544 na inaendelea kutoa huduma za matunzo katika makazi 13 ya wazee yanayomilikiwa na serikali.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima alisema katika kipindi cha 2022 hadi 2025 wizara hiyo imetoa huduma za msingi ikiwemo chakula, malazi, mavazi na matibabu kwa kushirikiana na sekta binafsi.
SOMA: Wazee watunzwe kulinda utu wa kila Mtanzania
“Wazee 1,256,544 wamepatiwa vitambulisho vya matibabu bila malipo pamoja na bima za afya kupitia programu za wizara,” alisema.
Alisema kupitia utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Wazee ya mwaka 2003, toleo la 2024, serikali imeanzisha mabaraza ya wazee 20,768 ifikapo mwaka 2025, ambayo yanatoa fursa kwa wazee kutoa maoni na ushauri katika masuala ya kijamii.
Sambamba na hilo, Dk Gwajima alisema serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa ushiriki wa wanawake katika uongozi na uwezeshaji wa kiuchumi kupitia mikopo kwa wajasiriamali waliosajiliwa.
Alisema jumla ya wajasiriamali 4,870 wamenufaika na mikopo yenye thamani ya Sh bilioni 9.9 huku kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake (WDF), wanawake wajasiriamali 45 wamewezeshwa mikopo yenye thamani ya Sh milioni 337.97 hadi Novemba 2025.
Aliongeza kuwa mwelekeo wa serikali katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ni kujenga taifa jumuishi lenye ustawi, haki na fursa za kiuchumi kwa makundi maalumu.
