MKURUGENZI Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Dk Peter Kisenge amesema taasisi hiyo imekuwa ikitoa msamaha wa takribani Sh milioni 200 kila mwezi kwa wagonjwa wa moyo wasiokuwa na uwezo
wa kugharamia matibabu.
Dk Kisenge alisema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ujio wa kambi maalumu ya
upimaji wa magonjwa ya moyo na magonjwa mengine yasiyoambukiza itakayofanyika jijini Arusha.
Alisema serikali ina utaratibu wa kusaidia wananchi wasio na uwezo kwa kufuata taratibu zilizowekwa ikiwemo kuandika barua kwa ustawi wa jamii na kufanyiwa tathmini.
“Taasisi imekuwa ikitoa msamaha wa Shilingi milioni 200 kila mwezi, hususani kwa watoto wenye matundu kwenye moyo. Mgonjwa anayefuata taratibu halali hukosa vikwazo vya kupata matibabu,” alisema.
Kuhusu kambi hiyo, alisema itaanza Desemba 29, 2025 hadi Januari 5, 2026 katika Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Center, ambayo imeingia ushirikiano wa miaka 20 na JKCI.
Alisema hadi sasa wamefanya upimaji katika mikoa 16 na kuwafikia wananchi zaidi ya 23,000 ambao asilimia 25 walibainika kuwa na matatizo ya moyo na asilimia tisa hawakuwa wanajua hali zao.
Alibainisha kuwa baadhi ya wagonjwa walihitaji kuwekewa vifaa vya kusaidia mapigo ya moyo vinavyogharimu takribani Sh milioni 10 lakini walipata huduma bure baada ya kugundulika mapema.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Tiba za Moyo JKCI, Dk Tatizo Waane alisema takribani asilimia 25 ya wagonjwa wanaofika JKCI hutoka mikoa ya kaskazini, hivyo kambi hiyo itarahisisha wananchi kupata huduma mapema.
