ARUSHA: ZAIDI ya wakazi 30,000 wa vijiji 11 vya Tarafa ya Engarenaibor wilayani Longido mkoani Arusha wameondokana na changamoto kusaka usafiri kwa mama wajawazito na watoto baada ya serikali kupeleka gari ya wagonjwa ya kisasa yenye thamani ya Sh milioni 350 katika kituo cha afya cha Engarenaibor kilichopo Longido mkoani Arusha.

Kituo cha afya hicho kinahudumia wakazi wa kata nne  zilizoko tarafa hiyo ambazo ni pamoja na Mundarara, Sinonik , Eangarenaibor na kata ya Matale iliyopo mpakani mwa nchi jirani ya Kenya na huduma ya afya katika kata hiyo ni changamoto kwani kutoka kata hiyo hadi Longido Mjini kupata tiba ni umbali wa zaidi ya km 130 hivyo kutolewa kwa gari hiyo ni mkombozi mkubwa kwa wakazi wa hiyo

Naibu Waziri wa Madini, Dk Steven Kiruswa alikabidhi gari hiyo na kusema kuwa serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imetoa gari hiyo yenye kila kitu ikiwemo huduma ya kwanza kwa kituo cha afya Engarenaibor baada ya kilio cha wananchi wa tarafa hiyo cha zaidi ya miaka 20 bila mafanikio na hivyo aliwaomba wananchi kumshukuru Rais kwa upendo wake wa kuwajali wananchi wa tarafa hiyo kwa kuwapa gari hiyo ya kisasa kwa ajili ya wagonjwa hususani akina mama wajawazito na watoto.

Dk Kiruswa alisema akina mama wajawazito wamekuwa wakipata taabu sana pindi cha kujifungua kwenda katika Hospitali ya Wilaya iliyopo Longido Mjini umbali wa zaidi ya km 40 na wengine walioppo mpakani husafiri umbali wa km 140 na kutokana na ujio wa gari hiyo itakuwa imewasaidia kwa kiasi kikubwa kuondokana na usumbufu huo na aliwaomba wahusika kutunza gari kwa maslahi ya wananchi wa Tarafa ya Engarenaiobor na maeneo mengine.

Akizungumzia baadhi ya changamoto katika tarafa hiyo ikiwemo maji, madarasa na madawati, Dk Kiruswa alisema ameanza kuzifanyia kazi yeye binafsi kwa kutoa fedha na pia ameshirikisha marafiki zake na tayari ameshanunuwa mabomba ya maji,ujenzi wa madarasa shikizi na ununuzi wa madwati ili wanafunzi waweze kupata elimu bora na sio bora elimu.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Longido mkoani Arusha, Salumu Kally amemwagiza Mwenyekiti wa Kijiji cha Engarenaibor na viongozi wengine wa serikali kuhakikisha wale wote waliojenga eneo la kituo cha afya na tayari wameshalipwa fidia kuondoka mara moja kwa hiari yao wenyewe.

Alisema inashangaza kuona watu waliomba kulipwa fidia kuendelea kubaki eneo la serikali wakati tayari wameshalipwa fedha na kwa kufanya hivyo ni kuikosea serikali hivyo wanastahili kuondoka haraka kabla ya kuondolewa kwa nguvu kwani kwani huo ni ukiukwaji wa makusudi.

Kally alizungumzia gari iliyopelekwa na serikali katika kituo cha afya Engarenaibor kwa kusema kuwa gari hiyo inapaswa kutunzwa kama mboni ya jicho kwani ni gari ya kisasa na kila mmoja anapaswa kuwa mlinzi wa gari hilo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha inafanya kazi iliyokusudiwa.

Naye Mganga Mfawidhi Kituo cha Afya Engarenaibor,Dk Paschael Mahenda aliishukuru serikali kwa kuwapatia gari hiyo ya kisasa kwa ajili ya mama wajawazito na watoto na kusema kuwa ni mkombozi mkubwa kwa wakazi wa kata hiyo ambao walikuwa wakisumbuka kwa ajili ya kusafirisha wagonjwa hususani wajawazito na watoto kwenda hospital ya wilaya kupata matibabu zaidi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *