Waziri Mkuu wa Sudan, Kamil Idris jana Jumatatu, alihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, na kuwasilisha mpango ambalo unajumuisha usitishaji mapigano kamili chini ya usimamizi wa kikanda na kimataifa, akisisitiza kwamba Sudan imelipa gharama kubwa kutokana na mzozo unaoendelea nchini humo.

Idris ameeleza kwamba mpango huo unalenga usitishaji mapigano kamili chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na Umoja wa Kiarabu, pamoja na kuhakikisha wanamgambo waasi wanapokonywa silaha.

Amesema kuwa mpango huo unajumuisha kutekelezwa programu za kupokonya silaha za waasi, na kutenganisha wapiganaji ambao hawakuhusika na utendaji jinai kwa lengo la kuwasaidia kurejea katika maisha ya kiraia, akisisitiza kwamba “hakuna amani bila uwajibikaji.”

Waziri Mkuu wa Sudan pia ametoa wito wa kuwepo mazungumzo kati ya makundi mbalimbali ya Wasudani katika kipindi cha mpito ili kukubaliana juu ya misingi ya utawala, huku awamu ya mpito ikihitimishwa kwa uchaguzi mkuu chini ya usimamizi wa kimataifa.

Kamil Idris amesema kwamba mpango huu ni “chaguo lililofikiriwa vyema la kubadilisha machafuko kuwa utulivu, vurugu kuwa sheria, na kukata tamaa kuwa matumaini,” akibainisha kuwa nchi yake imepitia kile alichokiita “uchokozi na wanamgambo wa kundi la RSF na waungaji mkono wake.”

Mateso ya binadamu nchini Sudan yanazidishwa na vita vinavyoendelea kati ya jeshi la taifa na wapiganaji wa Rapid Support Forces tangu Aprili 2023, ambavyo vimesababisha vifo vya makumi ya maelfu ya watu na kulazimisha wengine karibu milioni 13 kuhama makazi yao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *