
Dar es Salaam. Kila siku asubuhi katika maeneo mengi ya nchi, sauti mbalimbali husikika ambazo mara chache hupewa heshima ya kitaifa.
Ni sauti za nyundo zikigonga mbao kwa ustahimilivu, sauti za mashine za kukata mbao zikilia kwa mwangwi wa kazi.
Kwingine utaona cheche za mafundi wachomeleaji zikimulika anga la karakana ndogondogo, mashine za kushona nguo zikizunguka kwa kasi bila kuchoka na hata vijana ndani ya ovaroli wakiinamia magari mabovu.
Bila bahati, sauti hizi hazisikiki kwenye meza za uamuzi wa sera, wala hazionekani kwenye makabrasha mazito ya watoa zabuni, lakini ndizo sauti zinazojenga nyumba, shule, masoko, ofisi na miundombinu inayobeba maisha ya mamilioni ya Watanzania.
Ndani ya sauti hizi ndiko walipo mafundi mchundo, yaani watu waliobeba ujuzi mikononi mwao, lakini wamekosa vyeti vya darasani.
Kwa muda mrefu, mafundi hawa wamekuwa uti wa mgongo wa sekta nyingi muhimu, hususan ujenzi, useremala, uchomeaji wa vyuma na ushonaji.
Wamejifunza kazi si kwa kusoma vitabu, bali kwa kuangalia, kusikiliza, kujaribu na kukosea, hadi kufikia kiwango cha ubobezi kinachowawezesha kufanya kazi kwa viwango vinavyokubalika sokoni.
Pamoja na mchango wao mkubwa katika maendeleo ya Taifa, mfumo rasmi wa elimu na ajira haujawahi kuwatambua kikamilifu.
Hali hii imewafanya kubaki pembezoni mwa fursa nyingi za kiuchumi, hususan zile zinazotokana na miradi ya Serikali.
Safari ya ujuzi bila darasa
Simulizi ya mzee Juma Mtema (65) inaakisi maisha ya maelfu ya mafundi seremala nchini. Anafanya kazi katika eneo la Vingunguti jijini Dar es Salaam, mahali ambapo karakana ndogondogo zimekuwa shule zisizo na madarasa.
Anasema safari yake ya ufundi ilianza mapema alipolazimika kuacha shule ya msingi kutokana na changamoto za kifamilia.
Bila chaguo jingine, aliingia katika karakana ya jirani kama msaidizi mdogo; kazi yake ikiwa ni kubeba mbao, kufagia vumbi na kuwasha mashine.
Kadri muda ulivyopita, Mtema alianza kujifunza kwa macho na masikio. Alijua aina ya mbao kwa kuzigusa, alitambua vipimo sahihi bila kutumia rula, na alijifunza uvumilivu unaohitajika katika kazi ya mikono.
Leo, anaweza kutengeneza samani za kisasa, makabati ya ofisini, milango na madirisha ya hadhi ya juu bila mchoro wa kitaalamu. Amehudumia wateja binafsi, hoteli, taasisi za kidini na mashirika yasiyo ya kiserikali.
Hata hivyo, kila anapojaribu kuingia kwenye kazi za Serikali, safari yake huishia mezani.
“Wananiuliza cheti, si kazi,” anasema kwa masikitiko. Kwa mfumo wa sasa, uzoefu wake wa miongo kadhaa hauhesabiki bila uthibitisho wa kielimu unaotambulika kisheria, jambo linalomfanya ajihisi kana kwamba ujuzi wake hauna thamani mbele ya karatasi.
Si yeye pekee. Katika mitaa ya pembezoni mwa jiji hilo, Samuel Kalinga ni fundi ujenzi aliyepitia kila hatua ya kazi kwa vitendo.
Alianza kama mwandaa saruji, akawa mjenzi wa kuta, baadaye fundi paa na hatimaye msimamizi wa mafundi wengine.
Hajawahi kukanyaga chuo cha ufundi, lakini ana uwezo wa kusoma ramani za majengo kutokana na uzoefu wa muda mrefu.
Kwa miaka mingi, Kalinga ameshiriki kujenga shule binafsi, nyumba za ibada, majengo ya ghorofa na majengo ya biashara. Anaelewa misingi ya ujenzi, anajua hatari za kupuuza vipimo, na ana uzoefu wa kusimamia watu wengi kazini.
Hata hivyo, kila tangazo la zabuni ya Serikali linapopita, linakuwa kama ukumbusho wa kutengwa kwake. Vigezo vinamtaka awe na vyeti rasmi vinavyothibitisha taaluma yake, si historia ya kazi alizofanya kwa mafanikio.
“Ni kama mfumo unasema mchango wangu haupo,” anasema kwa uchungu. Hali hii imewafanya mafundi wengi kama yeye kubaki kwenye miradi midogomidogo, licha ya uwezo wao wa kutekeleza kazi kubwa zaidi.
Mwingine ni Hamisi Dotto, fundi chuma anayejulikana kwa kazi zake imara na salama. Ameunganisha milango ya chuma, madirisha ya ulinzi, ngazi za dharura na miundombinu mbalimbali ya viwandani.
Ana uelewa mkubwa wa aina za vyuma, mbinu za uchomeleaji na tahadhari za usalama kazini.
Kwa macho ya mteja binafsi, Ditto ni mtaalamu kamili. Lakini kwa macho ya mfumo rasmi, hana sifa zinazotambulika.
Amejaribu kushiriki miradi mikubwa kupitia makandarasi, lakini mara nyingi hukwama kwenye masharti ya nyaraka.
“Nina uzoefu, lakini uzoefu wangu haujaandikwa,” anasema. Cheche zake zinaonekana kazini, lakini hazionekani kwenye karatasi za zabuni.
Mfumo unaotukuza karatasi kuliko ujuzi
Changamoto ya mafundi mchundo hawa inaakisi mgongano mkubwa kati ya elimu rasmi na ujuzi wa vitendo.
Mfumo uliopo unathamini zaidi vyeti kuliko uwezo halisi, hali inayosababisha pengo kati ya kile kinachohitajika kisheria na kile kinachopatikana kwa uhalisia.
Matokeo yake ni kupotea kwa rasilimali watu wenye ujuzi mkubwa, huku miradi mingi ya umma ikitegemea idadi ndogo ya makandarasi wanaokidhi masharti ya karatasi.
Katika mazingira haya, mafundi mchundo wanaweza kujenga shule lakini hawawezi kupewa zabuni ya kuzijenga.
Urasimishaji wa mafundi mchundo si suala la huruma, bali ni mkakati wa maendeleo. Ni kutambua kuwa elimu ina njia nyingi, na kwamba ujuzi unaopatikana kwa uzoefu una thamani sawa na ule wa darasani.
Nchi nyingi zimeanzisha mifumo ya kutathmini na kuthibitisha ujuzi uliopatikana kwa vitendo kupitia vyeti vinavyotambulika kisheria.
Hatua hizi huongeza ajira, kupanua wigo wa makandarasi, kuboresha ubora wa kazi na kukuza uchumi jumuishi.
Matumaini yaja
Katikati ya mtanziko huo, kauli ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, imeibua matumaini mapya.
Waziri huyo anasema Serikali ina mpango wa kuwatambua na kuwarasimisha watu wenye ujuzi wa muda mrefu, ambao hawajapitia mfumo rasmi wa elimu, kupitia tathmini na vyeti vinavyotambulika kitaifa.
Mpango huu unatarajiwa kufungua milango kwa mafundi mchundo kushiriki katika zabuni za Serikali na fursa nyingine rasmi bila kubaguliwa kwa misingi ya historia ya elimu.
“Serikali inaendelea kuimarisha utaratibu wa kurasimisha ujuzi kwa vijana pamoja na watu wengine waliopata stadi mbalimbali nje ya mfumo rasmi wa elimu na kutoa fursa kwa wenye ujuzi wasio na vyeti vya taaluma ili waweze kutambuliwa na kutoa mchango wa kiuchumi,” alisema.
Prof. Mkenda anaunga mkono sera na mikakati ya serikali ya kutambua na kuwekeza katika ujuzi wa watu waliopata stadi nje ya vyuo vya elimu rasmi kama mafundi, wasanii, wakarabati magari, wajenzi, waashi, mafundi wa umeme na wengineo. kwa kuweka mwendelezo wa urasimishaji unaowapa fursa sawa na wale waliohitimu kwa njia ya elimu rasmi.
Kwa Mtema, Kalinga, Hamisi, Zalia na Habibu, urasimishaji si tu kupata karatasi, bali ni kupata heshima na haki ya kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa.
Kuwatambua rasmi mafundi mchundo ni kutambua historia hiy na ni hatua muhimu ya kuhakikisha hakuna ujuzi unaopotea kwa sababu haukupitia darasani.