Nuksi ya timu kukosa mikwaju ya penalti imeanza kuonekana katika Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 zilizoanza Desemba 21, 2025 nchini Morocco.
Katika mechi nne zilizochezwa hadi sasa, tayari penalti mbili zimeshakoswa jambo ambalo limezifanya timu zilizopoteza kutopata idadi nzuri ya mabao kwenye mechi husika.
Katika mechi ya ufunguzi, wenyeji Morocco walijikuta wakipoteza mkwaju wa penalti mapema katika dakika ya 11 dhidi ya Comoro.
Shuti la Soufiane Rahimi liliokolewa vyema na kipa wa Comoro, Yannick Pandor ingawa Morocco ilirekebisha makosa baadaye na kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 yaliyofungwa na Brahim Diaz na Ayoub El Kaabi.
Mchezo mwingine ambao penalti ilikosa ni ambao ulizikutanisha Mali na Zambia, Jumatatu, Desemba 22.
Dakika ya 42, Mali ilipata mkwaju wa penalti lakini ulikoswa na El Bilal Toure.
Pengine Toure angefunga penalti hiyo, Mali ingeibukana ushindi kwani filimbi ya mwisho ilipopulizwa, matokeo yalikuwa ni sare ya bao 1-1.
Bao la Mali lilifungwa na Lassine Sinayoko na bao la Zambia lilipachikwa na Patson Daka.
Mchezo huo wa Mali na Zambia ndio pekee ambao umemalizika kwa sare kati ya minne iliyochezwa katika mashindano hayo hadi sasa.
Matokeo ya mechi zilizochezwa AFCON 2025 hadi sasa
Morocco 2-0 Comoros
Mali 1-1 Zambia
Afrika Kusini 2-1 Angola
Misri 2-1 Zimbabwe