“TUNASHUKURU serikali imejitahidi kupitia vikao mbalimbali, wakiwemo wadau mbalimbali ambao ni madereva na matunda tunayaona. Luzicargo na tenki (malori ya mizigo yasiyo ya kontena) badala kwenda Sumbawanga Road wanavuka moja kwa moja, kilichobaki ni ‘container’ naamini magari yanayobeba makontena nayo yatapatiwa ufumbuzi.”
Anasema Rais wa Chama cha madereva cha Mkombozi Drivers African Group (MDAG) katika mazungumzo na gazeti la HabariLEO aliposhukuru na kupongeza serikali kwa utamaduni wake wa kuitikia na kutatua haraka kero za Watanzania zinapoibuka.
Alikuwa akiishukuru serikali kwa juhudi zake kutafuta na hata kuja na mbinu za kuondoa kero ya msongamano wa malori katika mpaka wa Tunduma baina ya Tanzania na Zambia akisema imekuwa ikiwaathiri vibaya madereva wa malori ya masafa marefu baina ya Tanzania, Zambia na nchi nyingine kupitia mpaka huo.
Vyanzo mbalimbali vinabainisha faida na umuhimu wa kiuchumi wa madereva wa sekta binafsi wakiwa wa malori ya masafa marefu wakiwamo wanaovuka mipaka ya nchi, vikisema ni pamoja na kukuza biashara ya kimataifa baina ya nchi na nyingine na kuongeza mapato ya serikali kupitia ushuru wa forodha, kodi za mafuta, ada za barabara na vibali.
Umuhimu mwingine ni sekta hiyo kutoa ajira kwa maelfu ya madereva, wasaidizi, mafundi, wahudumu wa maghala na mawakala wa forodha, kukuza sekta nyingine za uchumi na kuimarisha uhusiano wa kikanda.
Kutokana na kuridhishwa na hatua na juhudi za serikali kusikiliza kero za madereva hao na kuzitafutia ufumbuzi, Mkondo anasema MDAG hakuna sababu ya kuendelea na kusudio la kusitisha huduma lililopangwa kufanyika Januari Mosi, 2026 na badala yake watandelea kutoa huduma kuchochea ukuaji wa uchumi.
Anasema yapo mambo kadhaa yanayosukuma chama hicho kupongeza serikali kupitia Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Dk Mwigulu Nchemba, Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega na viongozi wengine wakiwamo wakuu wa mikoa ya jirani na Mpaka wa Tunduma unaotenganisha Tanzania na Zambia hasa Mbeya na Songwe.

Desemba 17, 2025 akiwa mkoani Songwe, Dk Mwigulu aliagiza kuvunjwa kwa ukuta wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), uliopo pembezoni mwa Barabara ya Tunduma ili ipatikane nafasi ya kupanua barabara hiyo inayotajwa kubeba uchumi wa Mkoa wa Songwe, ambayo imekuwa ikilalamikiwa kutokana na msongamano wa malori yanayoingia na kutoka nchini.
Anatoa agizo hilo kutokana na kilio cha ufinyu wa barabara hiyo kilichowasilishwa awali na Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Jabiri Makame aliyesema msongamano wa malori unasababishwa na ufinyu wa barabara. Nakala ya taarifa ya kuondoa kusudio la kusitisha huduma iliyolifikia gazeti hili Jumamosi iliyopita inasema,
“Ndugu zangu madereva wa nchi zote wanaovuka kutumia ‘Border’ (mpaka) ya Tunduma, Chama cha Madereva (MDAG) kilitangaza kusitisha huduma 01/01 /2026 endapo serikali haitashughulikia kero za madereva.”
Iliongezaa: “Tunashukuru serikali imejitahidi kupitia vikao mbalimbali, wakiwemo wadau mbalimbali ambao ni madereva na matunda tunayaona. ‘Loose cargo’ na ‘tank’ (malori ya mizigo yasiyo ya kontena) badala kwenda Sumbawanga Road wanavuka moja kwa moja, kilichobaki ni ‘container’ naamini magari yanayobeba makontena nayo yatapatiwa ufumbuzi.
“Na pia matunda mengine, Waziri wa Ujenzi alifika ‘border’ na Waziri Mkuu alifika. Wote kaulimbiu yao ni upanuzi wa barabara wakiwemo Mkuu wa Mkoa wa Songwe, RPC pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Momba. “Kwa matunda haya, kwa niaba ya madereva na vyama vilivyotuunga mkono leo 19/12/2025, natoa tamko rasmi hatutasitisha huduma 01/01/2026. Wenu Katibu Mkuu wa MDAG na Rais wa Group la African… Mkondo ahsante katika ujenzi wa taifa.”
Septemba 3, 2025 wakati akizungumza na wananchi wa Tunduma mkoani Songwea katika mkutano wake wa kampeni, mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan alisema serikali inapanga kuendeleza ukarabati na upanuzi wa barabara kuu inayounganisha Tanzania na Zambia, yenye urefu wa kilometa 75 ili kupunguza msongamano wa malori katika eneo la Mpaka wa Tunduma.
Rais Samia anasema upanuzi huo unalenga kuifanya iwe ya njia nne ili kurahisisha usafiri na usafirishaji na hatimaye kumaliza changamoto ya msongamano wa malori katika eneo hilo. Wiki chache kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 MDAG kilitoa mwito kwa Waziri Mkuu (Wakati huo alikuwa Kassim Majalia) kukutana na madereva wa sekta binafsi kujadili maendeleo, ufanisi na changamoto katika kazi zao.
“Tunaomba atupatie hadhi hiyo ili madereva wa sekta binafsi tumweleze changamoto zetu maana mchango wetu pia ni mkubwa katika uchumi wa nchi…” anasema Mkondo. Kwamba, madereva wa malori ya mizigo katika sekta binafsi yaendayo nchi jirani za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Zambia na Zimbabwe kupitia Mpaka wa Tunduma mkoani Songwe wanakumbana na changamoto mpakani.
Miongoni mwa adha wapatazo madareva hao wanapotekeleza majukumu yao ni kulazimishwa kutumia Barabara ya Sumbawanga hadi Chipata kabla ya kuvuka Mpaka wa Tunduma, hali inayowaathiri kwa kutumika mafuta ya ziada nje na kiwango wanachopewa na wamiliki wa malori hayo kisichohusisha safari hiyo ya mzunguko kabla ya kuvuka mpaka.
Ananukuliwa akisema: “Tunatoka Songwe lakini ‘parking’ (maegesho) ya mwisho Trans Cargo ni foleni hadi Round About (Barabara ya Mzunguko) ya Kilimanjaro ambayo ipo One Post Border. “Kabla ya kuvuka, unaambiwa utumie Barabara ya Sumbawanga hadi Chipata na kugeuza hadi Round About unakokutana tena na foleni ya hadi siku mbili hivi ndipo uingie border (mpakani)…”
Anasema: “Kuzunguka kule kunasababisha mafuta kuisha kabla ya safari maana kutoka Dar es Salaam unapewa mafura ya Dar- Congo (DRC), Dar- Zambia au Dar- Zimbabwe sasa ukienda hadi Chipeta na kurudi, unatumia zaidi ya lita 40, hivyo katika safari utaishiwa mafuta Kalungu au Isoka nchini Zambia.”
Anaongeza: “Kutoka Tunduma hadi Mpaka wa Isoka ni kilometa 50 na Kalungu hadi Isoka pia ni kilometa 50. Sasa mafuta yakikukatikia, tajiri anakuletea lakini ukirudi Dar, unafikia ‘lock up’ (lumande) kwa kudaiwa umeiba mafuta au unalipishwa au kufukuzwa kazi na kupoteza haki zako…”
Mkondo alisema madereva hao kupitia chama hicho cha MDAG, wanaomba na kuamini kuwa hadi Januari Mosi, 2026 zitakuwa zimeshughulikiwa na kupatiwa ufumbuzi wa haraka ili waendelee kufanya kazi kujenga uchumi wa nchi.
“…Hatuhitaji kwenda hadi Chipeta, Barabara ya Sumbawanga maana hiyo safari inatugharimu mafuta bila sababu na huko pia hakuna huduma nyingi muhimu kama vyoo vya umma wala ulinzi, ndiyo maana tunaibiwa mara kwa mara bila kupata msaada,” anasema.
Akifafanua taarifa hiyo, Mkondo anasema wameondoa kusudio hilo baada ya serikali kushughulikia kero za madereva na kwamba, mazungumzo na ustahimilivu ni mambo muhimu katika kujenga umoja, amani, maelawano na maendeleo katika nyanja mbalimbali zikiwamo za kiuchumi.
Kwa mujibu wa Rais huyo wa MDAG, hayo ni matokeo ya vikao vya majadiliano na ziara mbalimbali za viongozi hao akiwamo Waziri Mkuu, Dk Mwigulu kufika mpakani hapo na kaulimbiu ya upanuzi wa barabara.
Ajali na kero nyingine
MDAG inataja baadhi ya mambo yanayochangia ongezeko la ajali za barabarani zinazohusisha malori ya mizigo ya masafa marefu yakiwamo yanayokwenda nje ya nchi na mabasi yanayosafirisha abiria katika mikoa mbalimbali nchini.
Inasema ni pamoja na sharti la mamlaka za usafiri na usafirishaji nchi kavu kutaka madereva wa zamani wakasome kwa wiki mbili, hali inayofaya madereva wengine wenye uzoefu kushindwa kumudu gharama na kuamua kukaa nyumbani bila kazi.
“Madereva wa zamani wameendesha kwa miaka mingi; 15 na wengine hadi 20 au zaidi bila kusababisha ajali kwa vile wanalinda nidhamu na sheria katika kazi zao, sasa wanaambiwa wakasome wiki mbili… “Mtu huyo ni yule aliyejifunza udereva kwa vitendo kwa miaka miwili hadi mitatu na kupata uzoefu kiasi cha kufanyiwa usaili na majaribo na kupata leseni, ndiyo maana mamia kwa mamia ya madereva wazoefu wako mitaani na hiyo inalikosesha taifa madereva wazoefu wanaoweza kupunguza ajali na kuchochea ukuaji wa uchumi nchini…”
Kwa mujibu wa MDGA, si sahihi kupuuza au kubeza uzoefu wa madereva wa zamani kwa kuwa madereva hao ndio huwafundisha wapya na kuwapa sifa za kujiunga kwenye vyuo mbalimbali vya udereva vikiwamo Chuo cha Taifa cha Usafirishai (NIT), Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) na Chuo cha Polisi.
“Wanatuomba tuwasaidie tripu ya pili au tatu akishajua kupangua gia 12, anaomba kwenda kusoma akiwa na leseni yake ya ‘Class D’ (Daraja D) anafanya ‘interview’ (usaili) anaonekana ni dereva, anaanza masomo na mwisho anafanya test (jaribio) na kuafulu,” anasema Mkondo.
Anaongeza: “Lakini dereva huyu hana uzoefu wa milima mikubwa na mikali maana amejifunzia mjini kwenye milima midogomidogo, hivyo akifika kwenye mlima mkali, kupanda inakuwa shida na akiambiwa kushuka mlima (mteremko mkali), breki yake inakuwa ni ajali na vifo, mambo yanayosababisha hasara kwa jamii na taifa kwa kupoteza nguvukazi yake na mali.”
Mkondo anaiomba serikali akisema: “Mheshimiwa Rais Samia, tunaomba kuwe na kipindi cha mpito; madereva wa zamani wa miaka 15 hadi 20 iliyopita, waendelee kupewa leseni ili waendelee na kazi zao maana madereva wengi wako mitaani na wanaweza kuleta mfumuko wa halifu ukiwamo wizi.”
Kuhusu madereva wa mabasi, anasema wengi ni kisababisha cha ajali kwa kukiuka alama, miongozo, sheria na kanuni za usalama barabarani. Kwamba, wanapita magari mengine yakiwamo malori ya mizigo hata sehemu zisizoruhusuiwa kisheria ingawa wamesoma.
Anasema: “Sasa tunajiuliza hawa madereva wamesomea wapi?” Kuhusu usimamizi wa sheria, anasema kasumba ya baadhi ya maofisa wa usimamizi wa usalama barabarani kutoza faini magari yanayobainika kuwa na hitilifu yakiwa safarini kisha wakayaruhusu kuendelea na safari inachangia kutokea ajali nchini.
“Faini haiondoi kosa wala hatari ya kutokea ajali; gari lolote linapokamatwa kutokana na hitilifu hata
kama litapewa adhabu, lisiruhusiwe kuendelea na safari hadi tatizo lirekebishwe,” anaema.