KATIKA mwambao wenye utulivu wa Ziwa Nyasa mkoani Ruvuma, eneo ambalo mara nyingi husimuliwa kwa mandhari yake ya kuvutia, rasilimali za kipekee na watu wake wenye bidii, upepo wa matumaini umeanza kuvuma upya.

Sababu ni ziara ya kikazi ya Balozi wa Tanzania nchini Malawi, Agnes Kayola aliyewasili wilayani humo kusaka, kubaini na kuhamasisha matumizi ya fursa za kiuchumi zinazoweza kubadilisha Nyasa kuwa kitovu kipya cha maendeleo Kusini mwa Tanzania.

Ziara yake inaleta nguvu mpya, mjadala mpya na mtazamo tofauti; mtazamo unaotazama Nyasa si kama wilaya ya mpakani pekee, bali kama eneo lenye uwezo wa kuchochea uchumi wa taifa na kuunganisha Mkoa wa Ruvuma na Ushoroba wa Kusini na nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Uchumi unaotegemea ardhi, maji na juhudi za watu Akiwasilisha taarifa rasmi mbele ya balozi huyo, Mkuu wa Wilaya ya Nyasa, Peres Magiri anaelezea hali halisi ya uchumi katika wilaya yake.

“Asilimia 75 ya uchumi wa Nyasa unatokana na kilimo,” anasema Magiri na kuongeza kuwa, mazao yanayotawala mashamba ya wananchi katika Wilaya ya Nyasa ambayo ardhi yake haijaharibiwa na mbolea za kemikali kuwa ni pamoja na mihogo, mahindi, maharage na karanga. Mazao mengine ambayo ni hasa kwa biashara ni pamoja na kahawa na korosho.

Hata hivyo, kilimo si sekta pekee inayobeba maisha ya wakazi wa Nyasa. Uchumi wa eneo hilo pia unatiwa nguvu na shughuli za uvuvi wa samaki wa aina mbalimbali kutoka Ziwa Nyasa na uchimbaji wa madini. Nyingine ni utalii hususani katika Kisiwa cha Lundo chenye mandhari adimu wakiwemo samaki wa mapambo. Ndani ya ziwa hilo kuna aina 400 za samaki wa mapambo.

radi wa Ujenzi wa Bandari ya Mbambabay utakaounganisha Wilaya ya Nyasa na nchi jirani za Malawi na Msumbiji.

Mkuu wa wilaya huyo anataja sekta mpya zenye kasi kubwa kuchochea uchumi kuwa ni pamoja na usindikaji wa mazao, usafiri na usafirishaji pamoja na uwekezaji katika hoteli na huduma za wageni. Kwa mujibu wa Mwongozo wa serikali kuhusu uchumi jumuishi, Nyasa inatajwa kuwa miongoni mwa wilaya zenye uwezo wa kuchangia ukuaji wa sekta za kimkakati iwapo itawekewa na miundombinu bora.

Kutangaza na kuchangamkia fursa
Katika mkutano wake na wafanyabiashara mjini Mbambabay, Balozi Kayola anatoa ujumbe mzito na wa kuhamasisha kujivunia, kutangaza na kuchangamkia fursa mbalimbali za kiuchumi na uwekezaji zilizopo. “Ni wajibu wetu kuamini katika fursa zetu, kuzitangaza na kuzilinda. Hakuna atakayekuja kuwekeza kama
sisi wenyewe hatuoneshi moyo wa uzalendo na uthubutu,” anahimiza.

Anawataka wafanyabiashara kuimarisha usalama wa mitaji yao, kutumia fursa za kilimo na mazao ya ziwani kwa kufuata sheria na taratibu na kushiriki kwa ujasiri katika sekta ya usafirishaji na huduma za mipakani.

Kauli yake inasisitiza umuhimu wa kuweka mazingira mazuri ya biashara, sambamba na matumizi sahihi ya mfumo wa kisheria ulioundwa na serikali kupitia sera za biashara za taifa. Bandari mpya; mlango mpya wa uchumi.

Kauli inayovutia wengi katika ziara hiyo ni kuhusu ujenzi wa Bandari Mpya ya Mbambabay. Mradi huo unaogharimu zaidi ya Sh bilioni 80 unatajwa kuwa miongoni mwa miradi mikubwa ya kimkakati Kusini mwa Tanzania.

Kwa mujibu wa Sera ya Miundombinu ya Usafirishaji (2020), bandari kama hii zinatarajiwa kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa bidhaa ndani na nje ya Tanzania na kurahisisha biashara ya kimataifa hasa baina ya Tanzania na nchi jirani za Malawi, Msumbiji na Zambia.

Aidha, inatarajiwa kuchochea uwekezaji wa viwanda vya kuchakata mazao, samaki, matunda na bidhaa nyingine na hivyo, kuongeza mapato ya Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa na Mkoa wa Ruvuma kwa ujumla.

Neno la Balozi Kayola
“Bandari hii itakuwa moyo wa uchumi wa Nyasa. Itafungua biashara, kuongeza ajira na kuimarisha shughuli za viwanda.” Kwa mara ya kwanza, Wilaya ya Nyasa inapata nafasi ya kuunganishwa moja kwa moja katika ramani ya biashara za kikanda katika SADC kupitia mradi wa kimkakati wa Bandari ya Mbambabay.

Waombacho wafanyabiashara
Wakizungumza kwa niaba ya wenzao, Vincent Muli na Gabriel Mathius wanaiomba serikali kupitia balozi huyo kuangalia namna ya kuboresha mazingira ya biashara, hususani katika mipaka ya Tanzania na Malawi. Wanapendekeza kujengwa kwa Soko la Kimataifa la Nyasa litakalokuwa kitovu cha bidhaa kutoka Tanzania kwenda Malawi, Zambia na Msumbiji na kuimarisha miundombinu ya usafiri na ukusanyaji bidhaa.

Wanahimiza kuwepo kwa mikakati ya urahisishaji wa biashara kama ilivyoainishwa katika Sera ya Biashara ya Mwaka 2020. Wanasema soko hilo litafanya Wilaya ya Nyasa kuwa kituo cha kimkakati kwa biashara za mipakani, hatua itakayoongeza mapato kwa wafanyabiashara wilaya hiyo na Mkoa wa Ruvuma.

Biashara halali, hati sahihi
Katika ujumbe wake, Ofisa Uhamiaji wa Wilaya ya Nyassa, Albert Masao anasema wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla wahakikishe shughuli za mipakani zinafanyika kwa uadilifu.

Anawataka wafanyabiashara kutumia hati halali za kusafiria badala ya nyaraka za dharura, kufanya biashara kwa kufuata taratibu za kuvuka mipaka na kujiepusha na biashara haramu na uvushaji holela wa bidhaa. Wanasema hayo yanaendana na sheria za uhamiaji na kanuni za kudhibiti mipaka zinazolenga kulinda uchumi na usalama wa wananchi na mali zao.

Ushirikiano na taasisi zaserikali
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa, Khalid Khalif anahimiza wafanyabiashara kushirikiana na ofisi za biashara za wilaya, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na mamlaka nyingine za mipakani ili kufanya shughuli zao kwa ufanisi.

Anasema ushirikiano huo utawezesha kutatuliwa kwa changamoto zao kwa haraka, kuimarisha mapato ya serikali na kuweka misingi thabiti ya ukuaji wa biashara.

Kutoka fukwe za ziwa hadi miradi ya kimkakati
Balozi Kayola anatumia ziara yake wilayani Nyasa kutembelea maeneo mbalimbali yakiwemo ya fukwe za Ziwa Nyasa na mengine yenye fursa mpya ya uwekezaji hasa wa utalii.

Aidha, anazuru Kisiwa cha Lundo eneo linaloweza kubadilishwa kuwa kivutio cha kimataifa, eneo la uwekezaji wa kibiashara, ujenzi wa Bandari Mpya ya Mbambabay, ofisi za Idara ya Uhamiaji na kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na wafanyabiashara.

Nyasa na safari mpya kiuchumi
Ziara ya Balozi Kayola imefungua ukurasa mpya kwa Wilaya ya Nyasa. Kwa mara ya kwanza, maeneo ambayo kwa muda mrefu yalikuwa yakionekana kuwa ya pembezoni, sasa yanaangaliwa kama nguzo ya maendeleo ya kikanda. Kwa uwekezaji sahihi,

ushirikiano wa wafanyabiashara pamoja na utekelezaji wa sera za kitaifa, Nyasa inaweza kuwa moja ya nguzo kuu za uchumi wa Tanzania.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *