Akizungumza mjini Kiev, Zelensky amesema Urusi ina tabia ya kushambulia wakati wa sherehe za krismasi, huku akisema kwa sasa hali ni ngumu kutokana na taifa lake kukosa mifumo ya ulinzi wa anga. Ukraine itasherehekea rasmi krismasi Desemba 25, kama ilivyo kwa wakristo wengine, lakini kwa waukraine walio wengi wanaendelea kuisherehekea siku hiyo Januari 7 wakifuata desturi za madhehebu ya Wakristo wa Orthodox kama ilivyo pia nchini Urusi.
Katika hotuba yake rais Volodymyr Zelensky pia alisema anatarajia, timu yake ya wapatanishi kurejea Ukraine hii leo baada ya kuwa na mazungumzo ya kina na mjumbe maalum wa Marekani Steve Witkoff huko Miami, Florida, Akisema angelipenda kusikia hatua zilizopigwa katika mazungumzo yao ya kutafuta amani ya Ukraine huku akisisitiza kuwa Marekani lazima itoe shinikizo la kweli wa Urusi ili isitishe vita vyake Ukraine.
“Marekani lazima iseme wazi, kwamba kama sio diplomasia, basi kutakuwa na shinikizo kubwa. Tutaipa Ukraine silaha, tutaiunga mkono, Marekani itaweka vikwazo kikamilifu kwa uchumi mzima na sekta zote zinazipa Urusi fedha. Bila haitowezekana kabisa kufikia amani. Putin bado hajahisi aina ya shinikizo linalopaswa kuwepo.”
Kwa upande wake Witkoff alisikika akisema mazungumzo yalikwenda vizuri baada ya kuwa na majadiliano tofauti na pande hizo hasimu Urusi na Ukraine.
Urusi yashambulia miundombinu ya nishati Ukraine
Wakati hayo yakijiri Urusi hii leo asubuhi imevurumisha mabomu yake na kusababisha sehemu ya mji kukosa umeme huku nchi jirani ya Poland ambae ni mwanachama wa Jumuiya ya kujihami NATO akijipanga haraka kuilinga anga yake.
Kulingana na jeshi la anga la Ukraine, mapema leo alfajiri vingora vya kuashiria mashambulizi ya mabomu vilisikika karibu sehemu zote za nchi hiyo huku nyumba kadhaa zikiharibiwa madirisha kupasuka. Waziri wa nishati amesema umeme mara moja ulikatika mjini Kiev na meneo mengine mengi ya karibu.
Kwa upande wake meya wa Kiev, Vitali Klitschko, amethibitisha kuwa watu watatu walijeruhiwa katika mashambulizi hayo ya leo asubuhi. Katika eneo jengine la Zhytomyr maafisa huko walisema watu sita walijeruhiwa katika mashambulizi ya Urusi wakiwemo watoto wawili. Hali ya wakaazi wengi sio nzuri kwa sasa kutokana na msimu wa baridi huku umeme na mifumo ya joto ikisambaratishwa.
Urusi imekuwa mara kwa mara ikiishambulia gridi ya umeme ya jirani yake katika miaka yake takriban minne ya vita tangu ilipovianza Februari 24, 2022.
