
Umoja wa Ulaya umeonyesha mshikamano na Denmark na eneo la Greenland kufuatia tangazo la Rais wa Marekani Donald Trump la kuteua mjumbe wake maalumu katika eneo hilo.
Mkuu wa sera za nje wa EU Kaja Kallas ametangaza msimamo huo kupitia mtandao wa kijamii wa X na kueleza: “tunaendelea kuwa katika mshikamano na Denmark na Greenland. Greenland ni eneo linalojiendeshea mambo yake katika Ufalme wa Denmark. Mabadiliko yoyote ya hadhi hiyo ni ya kuamuliwa na watu wa Greenland na Denmark pekee”.
Kallas ameendelea kueleza katika ujumbe wake huo: “tunategemea washirika wetu wote kuheshimu mamlaka yao ya kujitawala na umoja wa ardhi zao na kufungamana na ahadi zao za kimataifa, zilizoainishwa -pamoja na kwengineko- katika Mkataba wa Umoja wa Mataifa na Mkataba wa NATO”.
Rais wa Tume ya Ulaya Ursula von der Leyen, yeye pia ameunga mkono matamshi hayo, akisema usalama wa eneo la Aktiki unabaki kuwa kipaumbele muhimu kwa Umoja wa Ulaya.
Katika ujumbe alioweka kwenye mtandao wa X, von der Leyen ameongezea kwa kusema: “tunasimama kwa mshikamano kamili na Denmark na watu wa Greenland”.
Hayo yanajiri baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kutangaza kwamba Jeff Landry, gavana wa Louisiana, atahudumu kama mjumbe maalumu wa Marekani huko Greenland.
Trump aliandika kwenye mtandao wake wa Truth Social kwamba Landry anatambua “jinsi Greenland ilivyo muhimu” kwa usalama wa taifa wa Marekani na ataendeleza kwa nguvu maslahi ya nchi hiyo ili kuhakikisha usalama wa washirika na ulimwengu mpana.
Greenland, ambalo ni eneo lenye mamlaka ya kujiendeshea mambo yake chini ya utawala wa Denmark, limevutia maslahi ya Marekani kutokana na nafasi yake ya kimkakati kijiografia na utajiri wake mkubwa wa rasilimali za madini.
Huko nyuma pia Trump alishatangaza kuwa, kuimiliki Greenland ni “hitajio mutlaki” kwa usalama wa kiuchumi wa Marekani, akiilinganisha na “mkataba mkubwa wa mali isiyohamishika.”
Zote mbili, Denmark na Greenland zimekataa mapendekezo yoyote ya kuliuza eneo hilo, na kutilia mkazo tena mamlaka ya utawala ya Denmark juu ya kisiwa hicho…/