Timu ya taifa ya soka ya Tanzania itakuwa na kibarua kigumu kwenye michuano ya AFCON 2025, itakapokuwa ikitupa karata yake ya kwanza kwenye mchezo wa ufunguzi wa Kundi C, dhidi ya Nigeria.
‘Taifa Stars’, ambayo inashiriki michuano hiyo mikubwa barani Afrika kwa mara ya nne katika historia yake ya soka, haijawahi kupata ushindi wowote katika michezo ya awali ya AFCON iliyofanyika mwaka 1980, 2019 na 2024.
Mara tatu ambazo Tanzania imeshiriki michuano ya AFCON, haijawahi kupata ushindi wowote, huku ikitolewa mapema kabisa, kwenye hatua za makundi.
Katika mechi saba walizocheza, Nigeria imeifunga Tanzania michezo minne na kutoka sare michezo mitatu, huku Tanzania ikishindwa kupata ushindi wowote.
“Pamoja na mazingira yetu magumu, bado tumechagua ushindi. Wanigeria tunawafahamu, Waganda tumeshacheza nao tunawafahamu vizuri tu, Watunisia tunawafahamu,” yalikuwa ni maneno ya Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo wa Tanzania, Paul Makonda baada ya kukutana na kikosi cha ‘Taifa Stars’ katika Barcelo Convention Center, jijini Fes, Morocco, ambako timu hiyo imeweka kambi ya maandalizi.