Mabao ya Omar Marmoush na Mohamed Salah yalitosha kuipa ushindi Misri na kukwepa kipigo baada ya kutanguliwa kwa bao moja dhidi ya timu ya Taifa ya Zimbabwe katika mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 yanayoendelea huko Morocco.

Ufuatao ni uchambuzi wa mambo sita katika mchezo huo:

Dakika 45 za kipindi cha kwanza

Katika mchezo huo uliofanyika kwenye Uwanja wa Adrar jijini Agadir, ulianza kwa kasi ambapo Misri ilifanya mashambulizi kadhaa kwenye lango la Zimbabwe lakini hayakuweza kuzaa matunda.

Misri ilionekana kuwa bora mwanzoni mwa mchezo ikitengeneza nafasi tatu za wazi ambazo hazikuweza kutumiwa kwa ustadi na mshambuliaji, Emam Ashour ambaye baadaye alifanyiwa mabadiliko dakika ya 34 baada ya kuonekana hayuko fiti akimpisha Mostafa Mohamed.

Dube kiboko yao

Mshambuliaji wa Zimbabwe, Prince Dube aliwashangaza Waarabu baada ya kufunga bao la uongozi kwa timu yake. Dube aliingia wavuni dakika ya 20 ya mchezo baada ya kumalizia kwa ustadi mkubwa pasi ya Emmanuel Jalai. Mshambuliaji huyo anayekipiga Klabu ya Yanga ameendelea kuwa mwiba mkali kwa Waarabu zikiwa zimepita wiki chache tangu atoke kuifunga Klabu ya AS FAR ya Morocco katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Licha ya kuondoka kipindi cha kwanza vichwa chini, Misri ilikuwa imeshapiga mashuti manne yaliyokuwa yamelenga lango na mashutu 11 iliyapiga ndani ya boksi la Zimbabwe lakini utulivu na nidhamu ya ulinzi iliwafanya Zimbabwe maarufu kama The Worrious kuondoka kifuambele.

Dakika 45 za kipindi cha pili

Kipindi cha pili kilipoanza, Misri ilianza kucheza kwa kasi ili kutafuta bao la kusawazisha ambapo iliendelea kufanya mashambulizi kwenye lango la Zimbabwe ambao walikuwa nyuma wakijilinda na kutoka kushambulia kwa kushtukiza lakini wakati huu wapinzani walikuwa makini wakijilinda na kushambulia.

Zimbabwe iliendelea kukaza na kuzuia baadhi ya mashambulizi makali ya Waarabu hao lakini dakika 19 zilitosha kuweka mizani sawa baada ya Marmoush kufunga bao la kusawazisha dakika ya 64 akitumia vizuri pasi ya Mohamed Hamdi.

Dakika za maumivu

Kwenye majukwaa ya uwanjani walipokuwa wamekaa Waarabu, wengi waliamini shuhuri imeisha kwani Zimbabwe ilionekana kuzuia mashambulizi vilivyo lakini nyota wa Liverpool, Mo Salah alifunga bao lililowapa Mafarao ushindi wa dakika za jioni. Makosa yaliyofanywa na beki wa Zimbabwe kumsahau Salah kwenye eneo la hatari ndiyo yaliwagharimu na kuwanyiwa hata pointi moja dhidi ya Mabingwa hao wa Kihistoria Afrika.

Kilichoibeba Misri

Zimbabwe ilionekana kuidhibiti Misri hata ilipopata bao la kusawazisha bado iliendelea kuzuia mashambulizi kwa utulivu na nidhamu kubwa, lakini kilichoibeba Misri kuibuka na ushindi katika mchezo wa jana ni ubora wa mchezaji mmoja mmoja. Licha ya kuwa na wachezaji wengi wanaochezea ligi ya Misri tofauti na mataifa mengine makubwa yenye nyota wengi wanaochezea ligi za Mataifa ya Ulaya na Uarabuni lakini bado walikuwa bora kuliko wachezaji wa Zimbabwe ambao wengi wanatokea ligi za Afrika.

Ilikuwa ni vigumu kuwazuia Marmoush na Salah ambao wametokea kwenye ligi kubwa ya England na yenye ushindani mkubwa duniani, wamecheza michuano mingi mikubwa ikiwemo Ligi ya Mabingwa Ulaya na wameshakutana na kila aina ya timu zenye wachezaji bora, hivyo changamoto waliyopewa na Zimbabwe bado haikutosha kuwazuia kutumia ubora binafsi.

Ukiachana na hao walikuepo wachezaji wengine wanaotoka kwenye timu bora hapa Afrika, wachezaji kama Trezeguet, Marwan Ateya, Mohamed Hany na Yasser Ibrahim kutokea Al Ahly bado walionekana bora ukilinganisha na baadhi ya wachezaji wa Zimbabwe kama Emmanuel Jalai, Daniel Msendami, Godknows Murwira na Washington Navaya ambao wanachezea ligi ya Zimbwabwe ambayo hata kwa ubora bado ipo nyuma dhidi ya ligi ya Misri.

Ushindani umeongezeka

Licha ya kupoteza mchezo Zimbabwe haikuonyesha unyonge kwa vigogo hao na badala yake ilicheza kwa kujiamini na nidhamu nzuri ya kuithibiti Misri ambayo ililazimika kupindua meza na kupata ushindi jambo ambalo halikutazamiwa kutokea kutokana na Zimbabwe kuonekana kuwa timu namba mbili kabla ya mechi kuanza.

Ubora wa vikosi umeonekana kuzipa timu kubwa matokea hadi sasa huku ikiwa ni tahadhali kwani timu nyingi za madaraja ya kati hazihofii mpinzani mkubwa, zinachofanya ni kuwaheshimu na kucheza mpira bila presha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *