Kaimu Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Miguel Gamondi amekiri hali ya hewa ya baridi nchini Morocco ni changamoto kwa baadhi ya wachezaji wa kikosi hicho.

Gamondi aliyasema hayo wakati akikiandaa kikosi hicho kukabiliana na Nigeria katika mechi ya kwanza Kundi C kwenye Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025.

Mbali na Nigeria, katika fainali hizo zinazofanyika Morocco, Tanzania pia ipo kundi moja na mabingwa wa AFCON 2004, Tunisia na jirani zake Uganda, huku ikilenga kufanya vizuri zaidi ikishiriki kwa mara ya nne baada ya 1980, 2019, 2023 na sasa 2025.

Akizungumza baada ya mazoezi ya juzi katika Chuo cha Soka cha Mohammed VI mjini Rabat, Gamondi alisema hali ya baridi imewaathiri baadhi ya wachezaji wa kikosi cha Stars, lakini akasisitiza haitatumika kama kisingizio.

“Siyo tatizo kwa sababu hali ya hewa ni sawa kwa kila timu,” alisema kocha huyo raia wa Argentina.

“Ni kweli sisi tumezoea zaidi hali ya joto na baadhi ya wachezaji wanapata shida kidogo na baridi, lakini tunapaswa kuzoea. Hata kule Cairo wakati wa kambi yetu ya mazoezi kulikuwa na baridi. Hii siyo sababu, ni sehemu ya kazi.”

Gamondi pia alieleza kuridhishwa kwake na maandalizi ya timu akisema: “Maandalizi yetu ni mazuri, mazingira hapa ni bora na tunafanya kazi kwa juhudi kubwa kuandaa timu kwa njia bora zaidi.

“Morali kambini ni nzuri sana. Tumejawa na furaha na hamasa kubwa kuiwakilisha Tanzania kwenye Kombe hili la Mataifa ya Afrika.”

Ikumbukwe kuwa, moja ya mada kuu kabla ya kuanza kwa mashindano haya ni hali ya hewa ya baridi nchini Morocco, hasa kwa timu zinazotoka maeneo yenye hali ya joto zaidi. Ingawa kwa ujumla hali ya hewa katika miji mwenyeji ni ya wastani, bado ni baridi ukilinganisha na mazingira ambayo timu nyingi za Afrika zimezoea.

Kwa kawaida, joto la mchana nchini Morocco huwa kati ya nyuzi joto 15 hadi 20, huku usiku kukiwa na baridi kali zaidi.

Mji wa Fes ambapo Taifa Stars jana ilicheza hapo na Nigeria, ni miongoni mwa miji yenye baridi kali zaidi, ikifikia nyuzi joto 14 mchana na kushuka hadi karibu nyuzi joto 6 usiku.

Kwa upande wa Mji wa Rabat ambao Taifa Stars mechi mbili zingine za kundi itacheza huko dhidi ya Uganda na Tunisia, ina hali inayofanana na na Casablanca, mchana inakadiriwa nyuzi joto 18 na usiku baridi, huku Tangier nayo ikiwa baridi kwa kufikia nyuzi joto 8 usiku. Lakini ukienda Marrakech na Agadir ni miji yenye joto zaidi, hususan Agadir ambayo hufikia hadi nyuzi joto 22 mchana.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *