
Mzikamaiti Yousef Abu Hatab mkazi wa Ukanda wa Ghaza na mmoja wa mashuhuda wa moja ya majanga makubwa zaidi kuwahi kutokea katika historia ya Palestina, amesema ameshiriki kuzika karibu miili 18,000 ya Wapalestina waliouliwa shahidi wakati wa vita vya kinyama na vya mauaji ya kimbari yaliyofanywa na utawala wa kizayuni wa Israel katika eneo hilo la Palestina.
Akionekana ameshika jembe mkononi mwake lililokongoka, Abu Hatab, mwenye umri wa miaka 65 anasema, alizika maiti moja baada ya nyingine zilizokuwa zikifikishwa katika mji wa kusini wa Khan Younis mpaka makaburi yalipojaa.
“Wakati wa vita, nilisimamia mazishi ya miili ya Wapalestina kati ya 17,000 na 18,000,” ameeleza mzikamaiti huyo.
Mzee huyo wa Kipalestina ameendelea kusimulia kwa kusema: “tulizika miili hiyo katika hali mbaya, katika makaburi ya halaiki, makaburi ya watu binafsi, na ndani ya hospitali, chini ya mashinikizo yasiyo na kifani kutokana na idadi kubwa ya vifo”.
Mzikamaiti huyo ambaye ametoa ushuhuda wake huo baada ya vita kusitishwa huko Ghaza tangu mwezi Oktoba licha ya Israel kuendelea kukiuka kila mara usitishaji huo, amesema: “wakati wa vita, tulikuwa tukizika kati ya miili 50 na 100 ya Wapalestina kila siku. Ingawa idadi hiyo imepungua hivi sasa, makaburi yangali yanapokea miili.”
Amesema, anakumbuka aliwahi kuzika miili ipatayo 550 ndani ya kaburi la muda katika Hospitali ya Nasser huko Khan Younis wakati kituo hicho cha tiba kilipozingirwa na jeshi la utawala wa kizayuni wa Israel mwaka jana.
Abu Hataba anasema, moja kati ya nyakati ngumu alizokabiliana nazo ilikuwa ni katika mwezi wa Julai wakati alipolazimika kufungua makaburi ya binafsi kwa ajili ya familia maalumu, ili kuzika miili ipatayo 1,270 huku kukiwa na mashambulizi ya mtawalia ya jeshi la kizayuni.
Kwa matukio hayo ya kusononesha na kusikitisha, Abu Hatab anasema, hawezi kusahau baadhi ya taswira zake wakati wa usiku.
“Kuna usiku ambapo huwa siwezi kulala kabisa,” ameeleza mzee huyo wa Kipalestina akiongezea kwa kusema: “sauti za mazishi, mayowe na miripuko hazisiti kichwani mwangu.”
Jeshi la utawala wa kizayuni wa Israel hadi sasa limeshawaua shahidi karibu Wapalestina 71,000, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, na kuwajeruhi zaidi ya 171,000 tangu Oktoba 2023 lilipoanzisha vita vya kinyama na vya mauaji ya kimbari dhidi ya Ghaza na kuligeuza eneo hilo kihame na magofu…/