Nigeria. Serikali ya Jimbo la Niger nchini Nigeria imeahidi kuwalinda watoto dhidi ya matukio ya utekaji katika kipindi hiki kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka za Krismasi na Mwaka Mpya.

Hayo yameelezwa jana Jumatatu Desemba 22. 2-25 wakati serikali ya jimbo hilo ikiwapokea watoto na walimu 130 waliotekwa nyara na kuachiliwa huru baada ya kuwa mateka kwa muda wa mwezi mmoja.

Utekaji wao kutoka shule ya bweni ya Kikatoliki katika jamii ya Papiri, Jimbo la Niger, ni miongoni mwa matukio makubwa ya utekaji katika historia ya Nigeria.

Hakuna mtu au kundi lililodai kuhusika na tukio hilo hadi sasa, lakini wakazi wa eneo hilo wanayalaumu makundi yenye silaha yanayotafuta fidia.

Utekaji nyara shuleni umekuwa ishara ya ukosefu wa usalama katika nchi yenye idadi kubwa zaidi ya watu barani Afrika. Sasa mamlaka zinasema zinaimarisha hatua za kiusalama.

Mratibu wa kitaifa katika Kituo cha Kupambana na Ugaidi cha Nigeria, Adamu Laka amesema wanatekeleza hatua za muda mfupi za ulinzi katika maeneo hatarishi dhidi ya watoto na jamii kwa ujumla.

Amesema wanakishirikiana na serikali za majimbo, viongozi wa kimila na wa kidini, ili kupata suluhisho la kudumu kwa ajili ya usalama.

“Elimu haipaswi kuathiriwa na vurugu. Tutaendelea kufuata sera na operesheni zitakazorejesha imani, kufungua tena shule kwa usalama na kuhakikisha kuwa haki ya kila mtoto wa Nigeria ya kupata elimu katika mazingira salama inalindwa,” amesema.

Hata hivyo, maafisa wa serikali hawajaweka wazi iwapo walilipa fedha zilizoombwa na watekaji au la ili kuachiwa watoto hao.

“Sidhani kama ni haki sana kwa mfumo au kwa serikali kuulizwa kama pesa zilitumika au la. Jambo la muhimu zaidi ni kwamba tumewarejesha watu hawa bila madhara,” alisema Gavana wa Jimbo la Niger, Mohammed Umar Bago, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jana.

“Mambo mengine ni yetu sisi, si yenu. Kwa hiyo jambo la muhimu zaidi ni kwamba tumewapata watoto waliopotea, na namna tulivyofanya hivyo, sisi tunaijua.”

Shule hiyo ilisema watoto wengi waliotekwa nyara walikuwa na umri kati ya miaka 10 na 17. Hivyo watoto hao wataungana na familia zao kwa ajili ya kusherehekea Sikukuu ya Krismasi na Mwaka Mpya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *