Rais Masoud Pezeshkian wa Iran amewasilisha rasimu ya bajeti ya mwaka ujao wa kifedha wa Iran (kuanzia Machi 21, 2026) katika Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran).

Serikali ya Pezeshkian imewasilisha muswada huo wa bajeti ya mwaka ujao wa Kiirani 1405 kwa mara ya kwanza kwa kuzingatia “rial mpya,” kufuatia kuondolewa kwa sifuri nne kutoka kwenye sarafu hiyo ya kitaifa.

Hatua hiyo, ikiwa itapokea kibali cha mwisho, inatarajiwa kutamatisha miaka mingi ya kutumia tarakimu kubwa na hesabu ngumu katika sarafu ya nchi hii.

Mkuu wa Shirika la Mipango na Bajeti la Iran, Hamid Poormohammadi amesema kwamba chini ya sheria mpya, muswada wa bajeti ya 1405 umewasilishwa Bungeni baada ya kupunguza sifuri nne kutoka kwenye sarafu.

Muswada wa bajeti ya mwaka ujao umeripotiwa kuandikwa sambamba na kitengo kipya cha fedha, huku vipengee vyote vya mapato na matumizi, mgao kwa vyombo vya serikali, na jedwali kuu za bajeti zikiwasilishwa kwa wabunge katika muundo mpya wa tarakimu.

Kwa mujibu wa kanuni za ndani za Bunge la Iran, serikali inapaswa kuwasilisha muswada wa bajeti ya kila mwaka Bungeni mwezi Desemba kila mwaka kwa ajili ya mapitio na idhini.

Mara tu wabunge watakapouidhinisha muswada huo, utapelekwa kwa Baraza la Katiba kwa ajili ya kupasishwa kuwa sheria.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *