Mbeya. Mbunge wa Mbeya Vijijini, Patali Shida amekabidhi mkopo wa Sh485 milioni uliotolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya kwa vikundi 15 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Hatua hiyo imetajwa kuwa ni utekelezaji wa agizo la Serikali kuwezesha makundi hayo kwa lengo la kuanzisha miradi endelevu ya kujikwamua kiuchumi.
Shida amekabidhi mkopo huo leo Jumanne Desemba 23, 2025 kwenye hafla iliyofanyika Stendi ya Tarafani katika Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mbalizi, wilayani Mbeya Vijijini.
“Mikopo hii ni kutimiza ndoto ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha kundi la vijana wanawezeshwa kiuchumi na kuanzisha miradi, lakini tumeshuhudia leo vikundi 15 vyenye watu 108 vimenufaika kwenye kata tisa kati ya 28,” amesema.
Ameonya tabia ya kuchukua mali za wananchi wanaoshindwa kurejesha mikopo, akieleza tafsiri yake ni kuwa maofisa maendeleo ya jamii hawakutoa elimu ya mikopo.
“Maofisa maendeleo ya jamii kabla ya kutoa mikopo toeni elimu ili kusaidia wananchi kurejesha kwa wakati, kitendo cha kutumia dhamana kuchukua mali ni dalili za kutotekeleza majukumu yenu, katika hilo sipendi yatokee,” amesema.
Vilevile, amewataka watendaji wa Serikali kuendelea kupambana kuongeza vyanzo na makusanyo ya mapato ya ndani ya halmashauri ili msimu ujao kuongeza idadi ya wanufaika.
Mbunge wa Mbeya vijijini, Patali Shida akizungumza na wananchi wa Mamlaka ya Mji wa Mbalizi , leo Desemba 23, 2025 wakati wa hafla fupi ya utoaji wa mkopo wa asilimi 10 kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Picha na Hawa Mathias.
“Tengenezeni utaratibu mzuri kuhakikisha sifa mnazopewa kusimamia utoaji wa mikopo ziendane na uhalisia kwa kuondoa urasimu,” amesema akieleza halmashauri hiyo imefanya vizuri kwa asilimia 60 ya utoaji mikopo.
Ofisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Mbeya, Abdul Yahaya, amesema katika kipindi cha miaka mitano vikundi 357 vyenye sifa vilipata mkopo kati ya hivyo, vya wanawake 175, vijana 163 na watu wenye ulemavu 19.
Amesema kwa mwaka wa fedha 2020/2021 mpaka 2025/2026, halmashauri imetoa mkopo wa Sh4.581 bilioni kwa vikundi 252 kati ya hivyo vya wanawake ni 114, vya vijana 126 na vya watu wenye ulemavu 12.
“Sambamba na hilo, jumla ya watu 3,345, kati ya hao 1,253, wanawake, vijana 2,062 na watu wenye ulemavu 30 wamenufaika na mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri,” amesema.
Amesema mikakati iliyopo ni kuhamasisha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kuunda vikundi vya kiuchumi vyenye miradi, hususani wa pamoja ili kunufaika na mikopo hiyo.
Mingine ni kutoa elimu ya kilimo biashara na kuongeza mnyororo wa thamani ya mazao wanayozalisha, usimamizi wa fedha, mali na kuweka akiba ya uendelezaji miradi ya vikundi vya ufugaji kibiashara wenye tija.
Mnufaika wa mkopo ambaye ni mfugaji wa sungura, Anna Jordan, amesema kikundi chao kimepata mkopo wa Sh30 milioni ambazo zitaongeza wigo wa ufugaji.