Mwimbaji wa Pop kutokea Marekani, Selena Gomez, 33, hatimaye ameweka wazi sababu ya mabadiliko ya sauti yake ambayo kwa muda mrefu yamekuwa yakizua mijadala miongoni mwa mashabiki wake.
Selena, mkali wa kibao cha Calm Down (2022), akizungumza kupitia Insta Live, alijibu swali la shabiki aliyekuwa akitaka kujua kwanini sauti yake imekuwa tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Akijibu swali hilo, Selena alisema mabadiliko hayo ya sauti wanatokana na hali yake ya kiafya kwa sasa huku akisisitiza kuwa hajali sana maoni hasi ya watu kuhusu hali hiyo.
“Wakati mwingine mambo hutokea. Koo langu huwa linavimba kwa ndani mara nyingine, na hilo ndilo linalosababisha mabadiliko ya sauti,” alisema Selena.
Mara kadhaa amekuwa wazi kuhusu changamoto zake za kiafya, hasa ugonjwa wa Lupus ambao unaweza kusababisha uvimbe unaoathiri viungo mbalimbali vya mwili, ikiwemo koo na mapafu, hali inayoweza kuathiri sauti.
Baada ya kauli hiyo, mashabiki walitoa maoni yao kwenye mitandao wakimsifu kwa ujasiri na uaminifu wake. Wengi walieleza kumuunga mkono na kumpongeza kwa kuzungumza wazi kuhusu hali yake bila aibu.
“Mimi ninafurahi ameweka wazi hili kwa sababu tulikua tukimjua kwa sauti yake, halafu ghafla ikabadilika sana na watu wakaanza kubuni mambo mengi. Natumaini atakuwa sawa” alieleza shabiki.
“Selena ni mfano wa kuigwa, kuzungumzia kwa wazi kuhusu mabadiliko ya sauti bila aibu inahitajika ujasiri mkubwa. Tunakupenda, endelea kuwa imara Malkia wetu,” shabiki mwingine alieleza.
Mwanzilishi huyo wa chapa ya Rare Beauty, amewahi kuzungumzia madhara mengine yatokanayo na lupus, ikiwemo kuongezeka uzito, hali inayosababishwa na matibabu yake.
“Ninapokuwa natumia dawa, huwa nahifadhi maji mengi mwilini, na hilo ni jambo la kawaida kabisa… Na ninapokuwa nimeacha dawa, uzito hupungua,” alisema Selena mwaka 2023 kupitia Insta Live.
Mwaka huo huo, alizungumza tena suala hilo katika kipindi cha Apple TV+ kiitwacho Dear ambapo alieleza baadhi ya watu walichukulia hali yake ya kuongezeka uzito kama fimbo ya kumchapia.
“Uzito wangu ulikuwa unabadilika mara kwa mara kwa sababu ya dawa fulani nilizokuwa natumia. Watu wakachukua hilo na kulifanya jambo kubwa… Ilikuwa kama wanasubiri tu kitu cha kunishusha,” alieleza.
“Nilikuwa nikidhalilishwa kwa kuongezeka uzito kwa sababu ya kuugua lupus,” alisema Selena, mwigizaji wa filamu, Only Murders in the Building (2021).
Hata hivyo, alikiri kuwa aliona aibu kunenepa na hiyo ni baada ya mashabiki wengi kumkeli mitandaoni kutokana na hali hiyo.
“Ningeingia mtandaoni na kuposti picha yangu na kusema sijali wanachosema, sikubaliani nao lakini muda wote nikiwa chumbani kwangu ningelia sana sababu hakuna anayestahili mambo hayo” alisema Selena.
Ikumbukwe Selena aliwahi kutajwa Billboard kama Mwanamke wa Mwaka mnamo 2017, huku Jarida la Time likimtaja kuwa miongoni mwa watu 100 wenye ushawishi mkubwa zaidi duniani kwa mwaka 2020.