Katika Ukanda wa Gaza uliyoharibiwa na vita, Attallah Tarazi mwenye umri wa miaka 76 anashikilia zawadi ndogo za Krismasi — soksi na skafu — kama ishara adimu ya shangwe ya sikukuu. Zawadi hizo zinamlinda dhidi ya baridi ya majira ya baridi ya Gaza na kumpa faraja ya kiroho.

Tarazi alijiunga na Wakristo wenzake wa Kipalestina kuimba nyimbo za Krismasi. “Kristo amezaliwa,” waliimba kwa Kiarabu, wakiongeza “Aleluya.” Maneno hayo yalijaa matumaini, hata kama mazingira yaliyowazunguka yalikuwa yamejaa uharibifu.

Krismasi mwaka huu inaadhimishwa wakati wa usitishaji vita dhaifu, uliotoa nafuu ndogo baada ya miezi ya mashambulizi makali. Hata hivyo, maumivu ya vita kati ya Israel na Hamas, pamoja na maisha ya watu waliolazimika kuhama makazi yao, yamepunguza sherehe nyingi za jadi.

Tarazi na Wakristo wengine wachache Gaza wanajaribu kunasa angalau chembe ya roho ya Krismasi, licha ya hali ya sintofahamu. Anasema imani yake ya Kikristo ndiyo iliyomsaidia kustahimili miaka ya vita.

“Ninahisi furaha yetu juu ya kuzaliwa kwa Kristo inapaswa kuzidi uchungu wote tuliopitia,” anasema.

Ameishi kwa zaidi ya miaka miwili katika eneo la Holy Family Church, ambako kikundi cha waumini na wanakwaya kimekuwa kikitembelea watu waliokimbia makazi yao msimu huu wa Krismasi.

Maeneo ya Palestina, Jiji la Gaza 2025 | Wakristo wapamba kanisa la monasteri kwa Mwaka Mpya
Wakristo wa Palestina wakipamba Kanisa la Latin Monastery katika Jiji la Gaza City, licha ya hali ngumu, kuelekea maadhimisho ya Krismas.Picha: Omar Ashtawy/SIPA/picture alliance

Krismasi kati ya maumivu na kumbukumbu za hasara

Kwa wengine, maumivu hayaepukiki. Kwa Shadi Abo Dowd, huu utakuwa Krismasi ya kwanza tangu kifo cha mama yake, aliyeuawa Julai wakati shambulio la Israel lilipopiga eneo hilo hilo la kanisa la Kikatoliki.

Israel ilieleza masikitiko na kusema tukio hilo lilikuwa ajali. Abo Dowd anasema mwanawe pia alijeruhiwa katika shambulio hilo, ambalo lilimuumiza pia padre wa parokia.

Abo Dowd, Mkristo wa Orthodox anayeadhimisha Krismasi Januari 7, anasema hatafanya sherehe zaidi ya ibada na sala. “Hakuna sikukuu,” anasema kwa huzuni.

“Maumivu bado yapo. Tunapo katika hali ya kutokuwa na amani wala vita,” anaongeza.

Licha ya kupungua kwa mashambulizi tangu usitishaji vita ulipoanza Oktoba, vurugu bado hazijaisha kabisa, huku Israel na Hamas zikishutumiana kukiuka makubaliano.

Vita, uharibifu na hali ya kukosa amani

Vita vilianza Oktoba 7, 2023, baada ya wanamgambo wa Hamas kuvamia Israel, kuua takribani watu 1,200 na kuteka nyara karibu watu 250. Mashambulizi ya Israel yaliyofuata yamesababisha vifo vya karibu Wapalestina 71,000 Gaza, kulingana na Wizara ya Afya ya Gaza.

Mashambulizi hayo yamesababisha uharibifu mkubwa na kuwafanya karibu watu milioni mbili kuhama makazi yao. Mvua kubwa za hivi karibuni zimefurika kambi za wakimbizi na kuangusha majengo yaliyokuwa tayari yameharibika.

Abo Dowd anasema anawaambia watoto wake: “Mungu huwapa mapambano magumu zaidi askari wake wenye nguvu zaidi.” Lakini anahofia mustakabali wa uwepo wa Wakristo Gaza, akisema kuondoka kwao kungekuwa janga kwa mshikamano wa kijamii.

Kwa Wafa Emad ElSayegh mwenye umri wa miaka 23, Krismasi haijisikii kama zamani. Ndugu na marafiki wengi wamekimbia Gaza wakati wa vita.

Maeneo ya Palestina, Jiji la Gaza 2025 | Mazishi ya waathiriwa Wakristo baada ya shambulio la Israel dhidi ya kanisa
Mashambulizi ya Israel yameua Wakristo kadhaa katika Ukanda wa Gaza.Picha: Dawoud Abu Alkas/REUTERS

Alisaidia kupamba mapambo katika eneo la kanisa la Orthodox la Kigiriki, lakini anakiri kuwa kukosekana kwa wapendwa wake kunazua huzuni na kumbukumbu nyingi.

“Tulikuwa pamoja katika kila kitu,” anasema, akiongeza kuwa shangwe ya Krismasi iliyojumuisha hata Waislamu sasa imepotea.

Furaha ndogo katikati ya maumivu makubwa

Kwa Elynour Amash mwenye umri wa miaka 35, mapambo ya mti wa Krismasi ni njia ya kuwapa watoto wake matumaini.

“Wanahisi furaha kidogo, kama kupumua baada ya kukosa hewa kwa muda mrefu,” anasema.

Ingawa anaishukuru nyumba yake bado imesimama, hali ya wakimbizi kwenye mahema baridi humfanya alie. Anasema mtoto wake mdogo hutetemeka anaposikia sauti kubwa.

Tarazi, licha ya kumpoteza dada yake na kaka yake wakati wa vita, anasisitiza kuwa ataendelea kubaki Gaza.

“Imani yetu na furaha juu ya kuzaliwa kwa Kristo ni kubwa kuliko hali zote,” anasema, akiiombea amani na uhuru Palestina.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *