Rukwa. Serikali ipo katika hatua za mwisho za kuanzisha kitengo maalumu kinachofanya kazi saa 24, kusikiliza maoni, mapendekezo na kero za wananchi, hususan kutoka kwa makundi maalumu, kwa lengo la kuimarisha ushirikishwaji, uwazi na uwajibikaji katika utendaji wa Serikali.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Clement Sangu, wakati wa kikao cha wadau wa mahusiano kilichofanyika leo, Desemba 23, 2025, katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa.

Akizungumza na Mwananchi Digital, Sangu amesema kitengo hicho kitarahisisha wananchi kuwasilisha changamoto zao moja kwa moja bila vikwazo vya kiurasimu, na pia kusaidia Serikali kupata mrejesho wa haraka ili kuboresha sera na huduma.

 “Kitengo hiki kitafanya kazi saa 24 kwa kuzingatia utu, haki na usawa” amesema Waziri Sangu.

Ameeleza kuwa kikao hicho kililenga kutambulisha majukumu ya Wizara ya Kazi, Ajira na Mahusiano, ikiwemo kuratibu mahusiano ya kisiasa na kijamii kwa kauli mbiu “Mahusiano Imara, Msingi wa Mshikamano wa Kitaifa.”

Akizungumzia ajira kwa vijana, Sangu amesema Makamishna wa Kazi wanapaswa kuhakikisha taarifa za fursa za ajira zinawafikia wananchi kwa wakati.

Sangu amebainisha kuwa mwaka 2025, vijana 5,118 ambapo wanaume walikuwa 3762 na wanawake 1256 walipata ajira za staha nje ya nchi kupitia Wizara yake.

Kuhusu Sekta Binafsi,  Sangu amesema kuanzia mwisho wa Januari 2026, kima cha chini cha mshahara kitaongezeka kwa asilimia 33.4, kutoka Sh275,060 hadi Sh358,322, akisisitiza kuwa utekelezaji wake ni wa kisheria na hatua zitachukuliwa kwa waajiri watakaokiuka.

Wadau wa mahusiano walioshiriki katika kikao hicho kilichofanyoka katika ukumbi wa mkutano katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa

Aidha, amewataka viongozi wa Mkoa wa Rukwa kushirikiana na madiwani kuhakikisha kuwa fursa za ajira, serikalini na sekta binafsi, zinawafikia wananchi kwa uwazi na usawa.

Kikao hicho kimesisitiza umuhimu wa mawasiliano ya uwajibikaji kati ya Serikali na wananchi, ili kuimarisha imani, mshikamano wa kitaifa na maendeleo jumuishi.

Baadhi ya washiriki wa kikao hicho, wakiwemo Lazaro Silas kutoka Chanji ambaye ni bodaboda, wameeleza kuwa watumishi wa umma wanapaswa kuwashirikisha vijana fursa mbalimbali zinazojitokeza katika maeneo yao, ili waweze kunufaika na fursa hizo.

“Vijana hatupati fursa zinawafikiwa wachache ambao wanandugu kwenye ngazi fulani tuliopo chini hatupati taarifa sahihi na hata tukijua tunakuwa tumechelewa,” amesema Silas.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *