
Imefahamika kwamba, Kocha Mkuu wa Simba, Steve Barker ndiye aliyependekeza Selemani Matola abaki kikosini hapo awe msaidizi wake katika benchi la ufundi analokuja kuliunda, huku akitaja sababu ya kufanya hivyo.
Ipo hivi; Desemba 19, 2025, Simba ilimtambulisha Barker kuwa kocha mkuu akitokea Stellenbosch ya Afrika Kusini akichukua nafasi ya Dimitar Pantev alitesitishiwa mkataba kwa makubaliano ya pande mbili Desemba 2, 2025.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Simba, kimeliambia Mwananchi kuwa, Matola ataendelea kufanya kazi na kocha huyo kama msaidizi wake namba mbili baada ya Barker kusisitiza anamuhitaji licha ya kwamba atakuja na wasaidizi wake wengine.
Mtoa taarifa huyo aliendelea kueleza kuwa, urafiki wa Barker na Matola wa siku nyingi ndiyo sababu ya kocha huyo Msauzi kupendekeza kuendelea kuwapo kikosini hapo kwani uzoefu wake wa kukaa na wachezaji muda mrefu utamsaidia kurahisisha kazi yake ya kuijenga Simba imara.
“Ni kweli Matola ataendelea kuwa sehemu ya benchi la ufundi, hii ni baada ya mapendekezo ya Barker kuomba kuendelea kufanya naye kazi na inaelezwa kuwa wawili hao walikuwa wanawasiliana hata wakati Fadlu akiwa kocha mkuu wa Simba,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;
“Atakuwa kocha msaidizi namba mbili kwani tayari Barker anamsaidizi wake ambaye atakuja naye siku chache zijazo tayari kwa ajili ya kuungana na timu, hivyo hakuna mpango wa kuachana na Matola kama ilivyokuwa inaripotiwa kuwa endapo kocha atakuja na benchi la ufundi atawapisha.”
Chanzo hicho kilisema msaidizi Barker, Matola na kocha msaidizi namba mbili anayekuja, wanafahamiana na walikuwa wakiwasiliana kabla hata ya mpango wa makocha hao kutajwa kutua Simba kuna dili walishauganishiana.
Inaelezwa kwamba, kiunganishi wa hayo yote ni aliyekuwa kocha wa Simba, Fadlu Davids ambaye hivi sasa anainoa Raja Athletic ya Morocco.
Baada ya Barker kubariki Matola kubaki kuendelea kuwa katika benchi la ufundi la Simba kama kocha msaidizi namba mbili, mzawa huyo ataendelea kuandika rekodi ya kufanya kazi na makocha wengi zaidi tangu mwaka 2019 alipotua Msimbazi akitokea Polisi Tanzania.
Katika miaka sita ya Matola akiwa kocha msaidizi Simba, amefanya kazi na chini ya makocha 10 tofauti, wakiwamo tisa wa kigeni na mmoja mzawa, timu ikitwaa mataji mawili ya Ligi Kuu Bara, Kombe la Muungano na Kombe la FA na kufika fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika iliyopoteza kwa RS Berkane ya Morocco kwa jumla ya mabao 3-1.
Simba inatarajiwa kurejea tena uwanjani mapema mwakani kwa mechi mbili mfululizo za Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Esperance iliyopo nafasi ya tatu kundini na pointi mbili na malengo ya klabu ni kutaka kocha mkuu mpya atue mapema aiandae timu sambamba na kufanya usajili wa dirisha dogo.