
Waziri Mkuu wa Libya Abdulhamid Dbeibeh ametangaza vifo vya mkuu wa majeshi na maafisa wengine wakuu kufuatia ajali ya ndege wakati wakirejea kutoka ziara rasmi nchini Uturuki.
Katika ujumbe kwenye mtandao wa X, Dbeibeh alisema siku ya Jumanne amepokea taarifa hizo “kwa masikitiko makubwa na huzuni,” akithibitisha kufariki kwa Luteni Jenerali Mohammad al-Haddad na waliokuwa kwenye ujumbe wake.
Miongoni mwa wale waliofariki pamoja na al-Haddad ni mkuu wa majeshi ya ardhini, mkuu wa mamlaka za viwanda vya jeshi, mshauri wa mkuu wa majeshi, na mpiga picha wa ofisi ya habari.
Waziri mkuu amesema tukio hilo limetokea wakati wakirejea kutoka mji mkuu wa Uturuki Ankara, bila kutoa maelezo zaidi kuhusu matukio hayo.
Akilitaja kuwa ni pigo kubwa kwa taifa na jeshi, waziri mkuu amesema Libya imepoteza watu waliokuwa wakitumikia nchi yao kwa nidhamu na dhamira kwa taifa,” akitoa salamu zake za rambirambi kwa familia, wafanyakazi wenzao jeshini na raia wa Libya kwa jumla.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uturuki Ali Yerlikaya awali alisema mabaki ya ndege hiyo binafsi iliyokyuwa ikielekea Libya iliyombeba mkuu wa majeshi ya Libya iliondoka jijini Ankara yalikuwa yamepatikana katika wilaya ya Ankara ya Haymana.
Awali waziri huyo wa Uturuki alisema mawasiliano yalipotea na ndege hiyo iliyokuwa imembeba mkuu wa majeshi ya Libya muda mfupi baada ya kuondoka kutoka uwanja wa ndege wa Esenboga jijini Ankara.