Taasisi kubwa zaidi ya Kiislamu nchini Misri ya Al-Azhar imesema, piganio la haki la Palestina limefikia kiwango cha dhulma na ukandamizwaji ambacho hakimruhusu mtu kubaki njiapanda na kudai kuwa haegemei upande wowote.

Kauli hiyo ya Al-Azhar imetolewa na Shekhe wake Mkuu Ahmed Al-Tayeb wakati alipompokea Bblozi wa Italia nchini Misri, Agostino Palese, katika makao makuu ya taasisi hiyo kuu ya Kiislamu nchini Misri.

Sheikh Al-Tayeb amesema, hali ya Palestina inahusisha kiwango kikubwa sana cha dhuluma na uchokozi unaohusu ukiukaji wa wazi wa tunu za ustaarabu, dini, ubinadamu na maadili, sambamba na kuendelea umwagaji damu, mauaji ya watoto, na jinai zilizofikia kiwango cha mauaji ya kimbari.

Shekhe wa Al-Azhar amebainisha kuwa, kinachotokea Palestina “hakiwezi kuelezewa kama vita, bali kama uchokozi na mauaji ya kimbari yanayofanywa na jeshi vamizi lenye silaha za kisasa kabisa dhidi ya watu wasio na silaha”.

Ameongezea kwa kusema: “tumepoteza wengi waliouawa shahidi wengi katika uchokozi huu wa kidhalimu, na tumeumizwa sana na damu ya watoto na wanawake. Hata hivyo, utawala ghasibu na wale wanaouunga mkono, nao pia wamepoteza, baada ya dhati yake halisi kufichuliwa mbele ya maoni ya umma duniani.”

Sheikh Al-Tayeb amebainisha kuwa, uga wa kimataifa unashuhudia mabadiliko ya wazi kabisa baada ya miaka mingi, ambapo dunia ilikuwa ikikubali simulizi ya utawala ghasibu kutokana na propaganda za uwongo na ushawishi mkubwa wa vyombo vya habari. Amesema watu katika nchi za Magharibi wamejitokeza mitaani kulaani mauaji ya Ghaza, wakiuelezea utawala huo kama msababishaji wa jinai mbaya zaidi dhidi ya ubinadamu, na kupelekea kuporomoka uungwaji mkono wake kwa watu.

Katika mazungumzo hayo na balozi wa Italia, Shekhe Mkuu wa Al-Azhar amewasifu pia wafanyakazi wa bandari ya Italia ambao walikataa kupakia silaha kwenye meli zilizokuwa zikipelekwa kwenda kutumika dhidi ya raia huko Ghaza, akikielezea kitendo chao hicho kama msimamo wa kiutu unaoakisi dhamiri hai na ubinadamu wa kweli…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *