Leo ni Jumatano tarehe 3 Rajab 1447 Hijria mwafaka na tarehe 24 Disemba 2025.
Siku kama ya leo miaka 1193 iliyopita yaani mwaka 254 Hijria, Imam Ali Naqi al-Hadi AS mmoja wa wajukuu wa Mtume Muhammad SAW aliuawa shahidi.
Alizaliwa mwaka 212 katika mji mtakatifu wa Madina. Alikua na kulelewa chini ya uangalizi wa baba yake, yaani Imam Jawad AS. Imam Ali al-Hadi alichukua jukumu la kuongoza Umma wa Kiislamu baada ya kuuawa shahidi baba yake.
Imam Ali al Hadi alitumia sehemu kubwa ya umri wake kufundisha, kulea wanafunzi na kueneza mafunzo sahihi ya dini tukufu ya Uislamu. Mapenzi ya watu kwa Imam Hadi kwa upande mmoja na elimu aliyokuwa nayo kwa upande wa pili, ni mambo yaliyowafanya watawala wa wakati huo wa ukoo wa Bani Abbas waingiwe na husuda, na ndio maana wakapanga njama za kumuua shahidi Imam huyo na kuitekeleza katika siku kama ya leo.

Miaka 501 iliyopita katika siku inayosadifiana na hii ya leo aliaga dunia Vasco da Gama baharia na mvumbuzi mashuhuri wa Kireno.
Vasco da Gama alizaliwa mwaka 1460. Mwaka 1498 baharia huyo mashuhuri wa Kireno alifanya kazi muhimu ya kuvumbua njia ya majini kutoka Ulaya hadi bara la Asia na India.

Miaka 176 iliyopita katika siku kama ya leo, majeshi ya Ufaransa yaliishambulia ardhi ya Guinea ya magharibi mwa Afrika.
Mashambulio hayo yalikuwa utangulizi wa Ufaransa kudhibiti ardhi hiyo iliyokuwa na utajiri wa dhahabu. Kabla ya vikosi vya Ufaransa kuishambulia ardhi ya Guinea, kulikuwa kumeanzishwa mashirika ya kibiasharaya dhahabu katika pwani ya Guinea.

Siku kama ya leo miaka 160 iliyopita, kundi la siri lililojulikana kwa jina la Ku-Klux-Klan ambalo liliitakidi kuwa watu weupe ni jamii ya watu bora na wa daraja la juu, liliasisiwa nchini Marekani kwa shabaha ya kupambana na watu wa jamii nyinginezo, hususan raia weusi.
Japokuwa kundi la Ku-Klux Klan lilipigwa marufuku miaka minne baada ya kuasisiwa kwake, lakini hadi kufikia sasa limeshafanya mauaji mengi dhidi ya raia weusi wa Marekani, kutesa, kuwaudhi, kuzusha hofu na kutoa vitisho dhidi yao.

Siku kama ya leo miaka 74 iliyopita Libya ilipatia tena uhuru wake baada ya kupasishwa azimio la Umoja wa Mataifa na Muhamad Idriss al Mahdi kuteuliwa kuwa mfalme wa nchi hiyo.
Huko nyuma Libya ilijulikana kwa jina la Tripoli na kwa miaka kadhaa ilikuwa chini ya himaya kubwa ya nchi za kigeni. Katika karne ya 16 Miladia Libya ilivamiwa na kukaliwa kwa mabavu na jeshi la Othmania. Aidha wakati wa kukaribia Vita vya Kwanza vya Dunia, nchi hiyo ilivamiwa na Italia lakini wananchi wa Libya wakapambana vikali na wavamizi hao wa Ulaya. Katikati ya Vita vya Pili vya Dunia, Uingereza na Ufaransa zikaikalia kwa mabavu nchi hiyo, na hatimaye Libya ikajipatia uhuru wake mwaka 1951.
