
Kesho Watanzania wataungana na watu wengine duniani kuadhimisha sikukuu ya Krismasi, siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Masiha, Mwokozi wa Wakristo, Bwana Yesu Kristo, aliyezaliwa zaidi ya miaka 2,000 iliyopita.
Ingawa Krismasi ni sikukuu yenye msingi wa Kikristo, kwa muda mrefu imekuwa ikiadhimishwa na kusherehekewa duniani kote na watu wa dini na mataifa mbalimbali, ikiwamo katika nchi zenye idadi kubwa ya Waislamu.
Hii ni kwa sababu Krismasi hubeba kile kinachoitwa “roho ya Krismasi” (the Christmas spirit), ambacho dhima yake kuu ni kutoa, kujitoa na kuonesha upendo kwa wengine.
Kihistoria, kuzaliwa kwa Yesu Kristo kulihusishwa na kuletwa kwa tumaini jipya kwa binadamu. Hata hivyo, katika maisha ya sasa, si lazima kuwe na kichanga kilichozaliwa leo ili kuadhimisha maana halisi ya Krismasi. Badala yake, ni wakati wa sisi Watanzania “kuzaliwa upya” kiroho na kimaadili, kwa kuamsha mioyo ya upendo, huruma na kujitoa kwa wengine.
Roho hii ya Krismasi inapaswa kuanza nyumbani, kwa familia zetu, majirani waliotuzunguka, ndugu, jamaa na marafiki, na hatimaye kuwafikia wazazi na ndugu walioko vijijini. Krismasi kimsingi ni sikukuu ya kutoa, si ya kupokea.
Utoaji huo unapaswa kuwa kwa wote bila ubaguzi wa dini, kwa sababu Krismasi, kwa mantiki pana, ni sikukuu ya wote. Katika Uislamu, Yesu anatambuliwa kama Nabii Issa bin Maryam, na sifa zake zinakubaliana kwa kiasi kikubwa na simulizi la Kikristo kuhusu Yesu Kristo.
Ingawa kila dini ina uhuru wa imani yake, ukweli kwamba Yesu anatambuliwa katika dini zote mbili kuu duniani unaonesha kuwa kuzaliwa kwake ni tukio lenye maana ya kipekee kwa binadamu wote.
Zaidi ya hayo, simulizi za mwanzo wa ulimwengu katika Ukristo na Uislamu zinafanana. Dini zote mbili zinakubaliana kuwa Mungu ndiye muumba wa ulimwengu na kwamba binadamu wa kwanza walikuwa Adam na Eva, au Adam na Hawa. Hivyo, wanadamu wote ni watoto wa baba mmoja, Adam. Hata maneno ‘mwanadamu’ au ‘binadamu’ yanatokana na dhana ya kuwa sisi ni wana wa Adamu.
Nembo ya Taifa letu inayoonesha mwanamke na mwanaume pia inaakisi wazazi hao wa kwanza wa binadamu.
Vilevile, Wakristo na Waislamu wanashirikiana simulizi la Nabii Abrahamu (Ibrahimu) na familia yake. Hadithi ya Abrahamu, mkewe Sara na mjakazi Hagai inaonesha masomo ya maisha, subira na imani.
Kupitia simulizi hilo, watoto wawili walizaliwa: Ishmaeli na Isaka. Katika mtazamo wa dini, Ishmaeli anahusishwa na chimbuko la Waislamu, huku Isaka akihusishwa na chimbuko la Wakristo. Pamoja na tofauti za tafsiri, simulizi hizi zinaonesha kuwa dini hizi mbili zinatoka katika mzizi mmoja wa imani kwa Mungu mmoja.
Katika ukoo huu ndipo alipozaliwa Nabii Musa, aliyewakomboa Waisraeli kutoka utumwani Misri na kupewa Amri Kumi za Mungu. Amri hizi ndizo hizo hizo zilizotambuliwa katika Ukristo, na Yesu Kristo alisisitiza kuwa hakuja kuzibatilisha bali kuzitimiza.
Hivyo, Wakristo na Waislamu wanashirikiana misingi ya maadili, sheria na imani kwa Mungu mmoja. Kwa msingi huo, kuadhimisha Krismasi kwa amani na mshikamano ni jambo linalowezekana na lenye tija kwa jamii.
Hata hivyo, changamoto kubwa kwa Watanzania wengi ni namna wanavyoisherehekea Krismasi. Wapo wanaojiandaa kwa mwaka mzima kwa kuweka akiba, lakini siku inapowadia, badala ya kuzingatia kutoa kwa wengine, hujikita zaidi katika matumizi makubwa ya anasa, kula, kunywa, kusafiri na kujizawadia wao wenyewe. Hali hii huipotosha maana halisi ya Krismasi.
Ni muhimu, katika kipindi hiki, kila mmoja akatafakari hali ya jirani yake. Watanzania hatufanani kwa kipato na uwezo wa maisha. Kuna wagonjwa hospitalini, wafungwa magerezani, yatima katika nyumba za watoto, pamoja na watu wengine wengi wenye mahitaji. Kuwatembelea, kuwafariji na kuwapatia chochote kidogo tulichonacho ni njia ya kudumisha roho ya Krismasi ya kutoa na kujitoa.
Kwa yote tuliyopitia kama taifa katika mwaka huu, Krismasi iwe fursa ya kuzaliwa upya kimaadili na kiroho. Tujenge upya misingi ya upendo, mshikamano na huruma.
Tukifanya hivyo, Krismasi haitakuwa tu siku ya sherehe, bali itakuwa mwanzo wa maisha mapya ya kupendana na kuishi kama ndugu, kwa sababu sisi sote ni familia moja ya binadamu.