Chanzo cha picha, Getty Images
Muda wa kusoma: Dakika 6
Katika miongo miwili iliyopita, Afrika imekuwa moja ya maeneo yanayokua kwa kasi kiuchumi duniani, ikiwa na wastani wa ukuaji wa Pato la Taifa wa kati ya asilimia 3.5 na 4.5 kwa mwaka. Kadiri tunavyoelekea 2026, matarajio ya ukuaji yameendelea kuwa mazuri.
Ripoti ya benki ya dunia ya 2024 inaonyesha kuwa eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahara lilikua kwa asilimia 3.8 mwaka huo, na inatarajiwa kufikia kati ya asilimia 4.1 na 4.3 katika kipindi cha 2026 – 2027. Hata hivyo, takwimu hizi za uchumi wa juu hazioneshi hali halisi ya watu wengi.
Zaidi ya waafrika milioni 460 bado wanaishi katika umaskini uliokithiri, wakiwa na kipato kisichozidi dola 2.15 kwa siku, kiwango kilicho juu kuliko ilivyokuwa miaka 15 iliyopita licha ya ukuaji.
Hili ni fumbo linalowatatiza wachumi: kwa nini uchumi unakua, lakini maisha ya wananchi wa kawaida hayaonekani kuboreka?
Hata katika nchi zinazofanya vizuri, kama Tanzania, Rwanda na Ethiopia, ukuaji unaonekana katika miundombinu, huduma za usafiri, uwekezaji wa miji na ukuaji wa sekta ya fedha.
Lakini kwa upande wa kaya maskini, gharama za maisha, mfumuko wa bei, mishahara duni na ajira zisizo na uhakika vinafanya rasilimali zisifika chini. Tofauti kati ya “uchumi wa namba” na “uchumi wa maisha” inaendelea kupanuka.
Tatizo hili lina mizizi yake katika mifumo ya kiuchumi, kijamii na kisera ambayo kwa miongo kadhaa imejengwa juu ya unyonyaji au utegemezi.
Hata nchi zinapopata mikopo au misaada mikubwa kutoka nje, mara nyingi fedha hizo hazibadilishi uzalishaji wa ndani bali huenda kulipia madeni, mishahara ya juu serikalini au miradi isiyo na matokeo makubwa kwa wananchi. Ndiyo maana, hata tunapokuwa na ukuaji, hauwi jumuishi.
Tunapoingia 2026, wachumi wa Afrika wanakubaliana: tatizo si kwamba Afrika haikui; tatizo ni kwamba haikui kwa namna ambayo inaondoa umaskini.
Kwa mantiki hiyo, mada hii haiepukiki: kwa nini takwimu za juu hazionekani kwenye mkoba wa mwananchi wa kawaida wa Afrika?
Ajira, idadi ya watu na gharama za maisha, mizizi ya umaskini unaogoma kupungua
Chanzo cha picha, Getty Images
Changamoto ya kwanza ni kwamba ukuaji wa Afrika hauzalishi ajira za maana. Benki ya dunia inaonyesha kuwa kwa kila asilimia 1 ya ukuaji wa pato la taifa Afrika, umasikini unapungua kwa wastani wa asilimia 1 tu, wakati wastani wa dunia ni zaidi ya asilimia 2.5.
Hii inaashiria kwamba uchumi wa bara unasukumwa zaidi na sekta zisizo na ajira nyingi, kama uchimbaji madini, utendaji wa serikali, au miamala mikubwa ya kifedha.
Kwa upande mwingine, sekta zinazoajiri watu wengi kama kilimo bado zina tija ndogo, hazina teknolojia ya kisasa, na hazina thamani ya juu yenye kuingiza fedha kwa wakulima. Japo kilimo kinachukua zaidi ya asilimia 55 ya ajira barani Afrika, kinachangia chini ya asilimia 20 ya pato la taifa katika mataifa mengi.
Zaidi ya hapo, idadi ya watu barani inaongezeka kwa kasi ya kipekee duniani. Kwa mujibu wa United Nations Population Division, bara linaongeza takriban watu milioni 30 kwa mwaka.
Hii ni neema ya nguvu kazi, lakini pia ni shinikizo la ajira, chakula, makazi, elimu na huduma za afya. Wakati uchumi unakua kwa asilimia 3.5, idadi ya watu inakua kwa karibu asilimia 2.7.
Kwa maana hiyo, faida ya ukuaji wa pato la taifa kwa mataifa husika inapunguzwa na idadi ya watu, na pato kwa mtu mmoja (GDP per capita) hubaki chini ya viwango vinavyoweza kubadilisha maisha. Ndiyo maana hata pale ukuaji unapoonekana, hali ya watu wengi hubaki ileile.
Gharama za maisha zimekuwa kikwazo kingine kikubwa. Ripoti ya Africa Pulse ya Aprili 2024 inaonyesha kuwa mfumuko wa bei kwa chakula katika nchi nyingi za Afrika Mashariki ulikuwa juu ya asilimia 20, huku bidhaa za msingi kama unga, mafuta ya kupikia, sukari na maharagwe zikifikia viwango vya juu zaidi ndani ya kipindi cha miaka saba.
Hii ina maana kuwa hata kama watu wanapata kazi, mishahara yao inaliwa na mfumuko wa bei.
Nchi kama Nigeria, Ghana, Ethiopia na Afrika Kusini zimekumbwa na kushuka kwa thamani ya sarafu, hali inayopandisha gharama za bidhaa zinazoagizwa kutoka nje. Matokeo yake ni kwamba uchumi unakua, lakini wananchi wanabaki bila mabadiliko halisi ya maisha.
Madeni akubwa, utegemezi wa nje na uwekezaji usiohimiza uzalishaji
Chanzo cha picha, Getty Images
Changamoto nyingine ni kwamba mataifa mengi ya Afrika yanategemea sana fedha kutoka nje kuliko ukuaji wa uzalishaji wa ndani. Takwimu za IMF za 2025 zinaonyesha kuwa zaidi ya nchi 20 barani ziko katika hatari ya kufilisika au tayari zinakabiliwa na mzigo mkubwa wa deni (debt distress).
Katika baadhi ya mataifa, zaidi ya asilimia 40 ya mapato ya serikali yanaenda kulipia riba na marejesho ya mikopo, badala ya kuwekeza katika huduma za kijamii au uzalishaji wa ndani. Kwa mfano, Ghana ilitumia zaidi ya asilimia 50 ya mapato yake ya ndani kulipia madeni mwaka 2024, hali iliyolazimu kufanyika kwa marekebisho makubwa ya kiuchumi.
Afrika Mashariki, nchi nyingi, ikiwemo Tanzania, Kenya na Uganda, zinategemea kwa kiwango kikubwa misaada au mikopo yenye masharti nafuu kufanikisha bajeti zao. Katika mwaka wa fedha 2024/25, Tanzania ilitegemea fedha za nje kwa karibu robo ya bajeti yake.
Kutegemea nje hakumaanishi tatizo, lakini linajenga muundo wa uchumi unaosimama kwa miguu isiyo yake. Wakati mikopo inapochelewa au masharti yanakuwa magumu, uwekezaji wa ndani unadumaa, ajira haziongezeki, na uzalishaji wa ndani haupanuki.
Tatizo pia ni aina ya uwekezaji unaoingia. Miji ya Afrika imeona miundombinu mikubwa: barabara mpya, madaraja, uwanja wa ndege, majengo marefu. Lakini miradi hii, ingawa ni muhimu, mara nyingi haizalishi ajira endelevu baada ya kujengwa; ajira nyingi ni za muda mfupi.
Bila sekta za viwanda, kilimo chenye tija, teknolojia na uzalishaji wenye thamani kubwa, Afrika itaendelea kuona ukuaji wa juu wa pato la taifa bila kupata manufaa kwa kaya za kawaida. Wachumi wanaita hali hii “jobless growth”ukuaji usiozalisha kazi.
Sera, utawala na usawa wa mapato mwisho wa mwisho wa fumbo la Afrika
Chanzo cha picha, Getty Images
Sababu ya mwisho inayozidisha tatizo ni utawala na usambazaji wa rasilimali. Ripoti za African Development Bank zinaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 65 ya utajiri mpya barani huenda kwa asilimia 10 ya watu walio juu kiuchumi.
Hii ina maana kuwa hata pale uchumi unakua, mgawanyo wa keki hauwi sawa. Ukosefu wa mifumo madhubuti ya kodi, uvujaji wa mapato, rushwa, na upendeleo wa kisiasa vinafanya fedha zinazopatikana zisinufaishe wengi.
Zaidi ya hapo, sera nyingi za kiuchumi barani zinategemea mipango ya muda mfupi badala ya mpango wa uzalishaji wa ndani wa miaka 20 na zaidi.
Ni vigumu kupunguza umaskini bila uchumi wa viwanda, bila mnyororo wa thamani wa kilimo, bila elimu stadi kwa vijana na bila mifumo ya kijamii inayowakinga watu masikini.
Hata pale serikali zinapoweka mipango bora, mara nyingi utekelezaji unakwamishwa na mabadiliko ya kisiasa, riba ya madeni, au ukosefu wa rasilimali.
Kwa maneno mengine: uchumi unakua juu, lakini unateleza chini kabla haujafika kwa watu.
Ndiyo maana, licha ya matarajio makubwa ya 2026, mustakabali wa kupunguza umaskini utategemea uwezo wa mataifa ya Afrika kubadilisha muundo wa uchumi wao si tu kuongeza ukuaji, bali kufanya ukuaji huo kuwa jumuishi, wenye ajira, wenye tija na wenye usawa.
Kadiri tunavyosogea kuelekea 2026, picha inaonekana wazi: Afrika inakua kimahesabu, lakini sio kimaisha.
Tatizo si kasi ya ukuaji, bali ubora wake. Swali pekee lililosalia ni hili, Afrika inaweza kukua, lekini inaweza kuwafanya watu wake kuwa matajiri?