Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) lina wasiwasi kuhusu kuibuka tena kwa vurugu katika mkoa wa Kivu Kusini. Katika taarifa iliyotolewa siku ya Jumanne, Desemba 23, shirika la Umoja wa Mataifa liliomba dola milioni 67 zifadhiliwe kwa dharura ili kudumisha usaidizi wake katika miezi mitatu ijayo.

Imechapishwa:

Dakika 1 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

WFP pia ilionyesha kuwa inahitaji dola milioni 350 ili kuendelea na shughuli zake nchini DRC. Hii ni pamoja na wito wa dola milioni 39 kwa Burundi na dola milioni 17 kwa Rwanda, huku kukiwa na ufadhili mdogo unaotishia kusitisha misaada ya kuokoa maisha kwa mamilioni ya watu.

Ingawa akiba ya chakula imepangwa katika baadhi ya maeneo yaliyoathiriwa, WFP inaonya kwamba bila rasilimali za ziada za haraka, shughuli zake zinaweza kuvurugika haraka. Kulingana na shirika hilo, watu milioni 2.8 tayari wanakabiliwa na ukosefu wa usalama wa chakula katika mkoa huo, ikiwa ni pamoja na karibu milioni moja katika hali za dharura. Kufikia mwezi Januari 2026, idadi ya watu walioathiriwa inaweza kuongezeka mara saba. “Mgogoro huu wa chakula una hatari ya kuwa mbaya zaidi ikiwa hatua za haraka hazitachukuliwa,” ameonya Cynthia Jones, kaimu mwakilishi waWFP nchini DRC, katika taarifa.

Ghasia hizo pia zimesababisha kuhama kwa wakimbizi kwenda nchi jirani. Nchini Burundi, WFP inawasaidia wakimbizi wapya wa Kongo wapatao 94,000 kwa kusambaza milo ya moto katika katika makambi ya muda. Nchini Rwanda, hadi watu 1,000 wamepokea msaada wa dharura wa chakula na lishe.

Hata hivyo, shirika hilo linaonya kwamba nafasi yake ya kufanya shughuli zake haipo kabisa. Siku ya Jumatatu, WFP ilitangaza kuwa imepunguza mgao wa chakula kwa wakimbizi nchini Burundi kwa 75%. “Bila msaada wa dharura na ufadhili wa ziada, hatuwezi kukabiliana na mgogoro ambao uko karibu na janga la chakula,” anabainisha Cynthia Jones kulingana na Radio OKAPI.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *