Timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ imeshindwa kuvunja mwiko baada ya kupoteza kwa mara nyingine dhidi ya Nigeria ‘Super Eagles’ katika mechi ya kundi C ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 yanayoendelea nchini Morocco.
Stars imeruhusu kufungwa mabao 2-1 huku ikishindwa kuvunja mwiko wa kufungwa na ‘Super Eagles’ tangu ilipofanya hivyo mara ya mwisho mwaka 1980 Nigeria ilipokuwa mwenyeji wa mashindano.
Ufuatao ni uchambuzi wa mambo saba yaliyoifanya Tanzania kuwa bora na kuzidiwa wakati wa mchezo;
Dakika 45 za kipindi cha kwanza
Katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa FEZ, Stars ilianza mechi kwa kasi kwenda kwenye lango la Nigeria lakini ilizuiwa na wapinzani wake walioonekana kuwa bora zaidi baada ya kuanza kumiliki mpira na kuanza kucheza kwa mipango kulielekea lango la Tanzania.
Katika dakika ya nane Nigeria ilikosa bao ambapo kipa wa Tanzania, Zuberi Foba aliweza kudhibiti mchomo uliopigwa na Akor Adams.
Stars nayo ilifanya shambulizi moja la hatari ambapo mshambuliaji, Simon Msuva aliachia shuti kali ambalo lilidhibitiwa na kipa wa Nigeria, Stanley Nwabali.
Dakika 36 zilitosha kuifanya Nigeria kupata bao la kuongoza baada ya beki, Semi Ajayi kuruka juu na kupiga mpira wa kichwa uliopigwa Krosi na Alex Iwobi.
Hadi dakika 45 za kipindi cha kwanza zinamalizika Nigeria iliondoka kifuambele ikiwa imepiga jumla ya mashuti 13, saba yakilenga lango wakati kwa upande wa Tanzania ilikuwa imepiga jumla ya mashuti manne huku mawili yakilenga lango.
Dakika 45 za kipindi cha pili
Kipindi cha pili kilianza Nigeria ikionekana kuanza kwa kasi ikifanya shambulizi la hatari kwenye lango la Stars dakika ya 46 ambapo mshambuliaji wao hatari, Victor Osimhen akifunga bao ambalo lilikataliwa na VAR baada ya kugundua kuwa alikuwa ameotea.
Stars ilicheza kwa nidhamu bila presha ya kumuogopa mpinzani wake. Kiungo Novatus Miroshi alithibitisha kwanini anacheza soka la kulipwa Uturuki baada ya kuachia pasi iliyomkuta Charles M’Mbombwa ambaye alimalizia kwa ustadi mkubwa na kuisawazishia Tanzania dakika ya 50.
Zilipita dakika mbili Ademola Lookman akairudisha tena Nigeria kwenye uongozi baada ya kutumia vizuri pasi ya Iwobi kwa kuachia shuti kali lililozama moja kwa moja wavuni.
Stars iliendelea kucheza kwa kushambulia na kujilinda lakini ilipata wakati mgumu kuvuka ukuta wa Nigeria ambao unaundwa na wachezaji wakomavu.
Hata hivyo, ilifanikiwa kupata nafasi kadhaa mwishoni mwa mchezo ambazo ilishindwa kuzitumia vyema na kufanya mchezo umalizike kwa kupoteza mabao 2-1.
Miroshi na M’Mbombwa walivyojikaza
Kipindi mchezo unaanza kiungo wa Stars, Miroshi hakuonekana kulidhibiti eneo la kati vizuri. Viungo wa Nigeria Iwobi na mwenzake Wlfred Ndindi walionekana kulishika eneo hilo vizuri kwa kuzuia na kuanzisha mashambulizi yalioenda pembeni na katikati kumwelekea Osimhen.
Miroshi anayekipiga Göztepe ya Uturuki alionekana bora sana kipindi cha pili akizuia na kutoa pasi zilizofika kwa uhakika kwenye maeneo mbalimbali hadi alipotengeneza bao la kusawazisha bado alizidi kun’gaa kwenye eneo hilo, licha ya viungo wa Nigeria nao wakionekana kucheza kwa viwango katika eneo hilo la kati.
Osimhen mambo magumu
Mshambuliaji huyo anayekipiga Galatasaray nchini Uturuki alipata wakati mgumu dhidi ya mabeki wa Stars, Bakari Mwamnyeto na Ibrahim Bacca walimdhibiti vizuri nyota huyo ambaye alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa ligi ya Uturuki. Hata hivyo, mshambuliaji huyo aliendelea kuzidiwa ujanja na walinzi wa Stars hadi alipofanyiwa sabu dakika ya 86 kumpisha Paul Onuachu, Osimhen alitoka uwanjani bila kutikisa nyavu za Tanzania.
Foba amekomaa
Golikipa wa Stars, Zuberi Foba licha ya kuruhusu mabao mawili lakini ameonyesha ukomavu wa hali ya juu baada ya kuokoa michomo kadhaa iliyopigwa kwenye lango lake.
Osimhen ni mmoja ya nyota wa Nigeria ambaye kama isingekuwa ubora wa Foba pengine angeondoka na bao kwenye mechi ya hiyo, lakini utulivu na mahesabu mazuri langoni yalimfanya apate wakati mgumu wa kuandika bao lake la kwanza kwenye michuanoo ya mwaka huu.
Uzoefu alioupata akiwa na Azam FC kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu, umemfanya golikipa huyo kuwa imara langoni tofauti na kipindi cha nyuma.
Kilichoibeba Nigeria
Uzoefu na komavu wa wachezaji ndiyo umeifanya Nigeria kuondoka na matokeoa ya ushindi. Wachezaji kama Osimhen, Lookman, Iwobi, Ndindi, Chukwueze na Adams hawa ni miongoni mwa nyota wenye uzoefu mkubwa wakiwa wameshiriki katika mashindano makubwa hivyo haikuwa rahisi kuweza kukabiriana nao.
Ubora wa mchezaji mmoja mmoja bado ulionekana kuibeba Nigeria kwa kiasi kikubwa. Licha ya kuondoka bila ushindi Tanzania haikuonyesha unyonge kwa vigogo hao wa soka Afrika.
Mwendo bado ujaisha
Stars inapaswa kujipanga upya katika mechi mbili zijazo ambapo itakabiriana na Uganda, Desemba 27 kabla ya kukutana na Tunisia, Desemba 30 mwaka huu.
Kiwango ilichokionyesha jana licha ya kupoteza mchezo kimetosha kuiombea mazuri katika michezo inayokuja kwani hata matokeo ya ushindi yanaweza kuiweka pazuri Tanzania na kuandika rekodi ya kushinda kwa mara ya kwanza tangu ilipoanza kushiriki mashindano haya mwaka 1980.