Chanzo cha picha, Getty Images
Muda wa kusoma: Dakika 5
Jesse Romero, Mkatoliki na mtangazaji wa kipindi cha mtandaoni mwenye msimamo mkali, ana maneno machache ya kuhusu Papa Leo XIV.
“Papa anapaswa kutuambia jinsi ya kufika mbinguni. Hana mamlaka juu ya serikali; lazima abaki katika njia yake.”
Ni mfuasi wa Donald Trump, amekasirika kuhusu ukosoaji uliofanywa na Papa mzaliwa wa Marekani na maaskofu wa Marekani kuhusu sera ya kuwafukuza wahamiaji.
Mmoja kati ya Wamarekani watano anajitambulisha kuwa ni Mkatoliki. Wakatoliki maarufu katika serikali ya Trump ni kama vile Makamu wa Rais JD Vance, Waziri wa Mambo ya Nje Marco Rubio, na Waziri wa Elimu Linda McMahon.
Lakini suala la uhamiaji limekuwa tatizo kati ya Kanisa na serikali, na pia miongoni mwa waumini wenyewe.
Papa Leo XIV amezungumzia mara kwa mara wasiwasi wake kuhusu jinsi wahamiaji wanavyotendewa nchini Marekani, mwezi Novemba alitaka “tafakari ya kina ifanyike” kuhusu jambo hilo.
Papa alirejelea injili ya Mathayo, na kusema “Yesu anasema waziwazi, mwishoni mwa dunia, tutaulizwa, ‘Mlimpokeaje mgeni?”
Wiki moja baadaye, Mkutano wa Maaskofu Wakatoliki wa Marekani (USCCB), ulitoa “Ujumbe Maalum” usio wa kawaida ukielezea “wasiwasi wao kuhusu hali inayobadilika inayowaathiri wahamiaji nchini Marekani.”
Maaskofu walisema “wamefadhaishwa” na kile walichokiita “hali ya hofu na wasiwasi.” Waliongeza kuwa “wanapinga kufukuzwa kwa watu ovyo” na “wanataka kukomeshwa kwa kauli na vurugu zinazodhalilisha utu.”
Ni uingiliaji kati usio wa kawaida, kwa mara ya kwanza USCCB kutoa taarifa kama hiyo katika kipindi cha miaka kumi na miwili. USCCB unamuunga mkono Papa, ambaye aliita kauli hiyo kuwa “muhimu sana” na akawasihi Wakatoliki wote na “watu wenye nia njema, kuisikiliza kwa makini.”
Vita na Papa
Chanzo cha picha, Getty Images
“Nadhani uhusiano huu ni mgumu sana,” anasema David Gibson, mkurugenzi wa Kituo cha Dini na Utamaduni cha Chuo Kikuu cha Fordham.
Wahafidhina walikuwa na matumaini Papa Leo angeleta mabadiliko kutoka mtazamo wa mtangulizi wake Papa Francis kuhusu masuala ya haki za kijamii na uhamiaji, kulingana na Gibson.
“Wengi wao wamekasirika. Wanataka kuliambia kanisa linyamaze,” na kujikita tu katika masuala kama vile utoaji mimba, anasema Bw. Gibson.
Tom Homan afisa wa Ikulu ya White House, anayeongoza sera za kuwafukuza wahamiaji – mwenyewe ni Mkatoliki – amesema Kanisa “limekosea,” na viongozi wake “wanahitaji kutumia muda wao kurekebisha Kanisa Katoliki.”
Mwezi Oktoba, Msemaji wa Ikulu ya White House Karoline Leavitt alipinga ukosoaji wa Papa mzaliwa wa Chicago, jinsi Marekani inavyowatendea wahamiaji kuwa “isivyo ya kibinadamu” na haiendani na itikadi ya kutetea maisha.
Gibson anasema kwa mujibu wa hesabu ya serikali “kuna Wakatoliki wa kutosha Marekani, hasa Wakatoliki Wazungu, wanaounga mkono Chama cha Republican na Donald Trump, na kuna faida kisiasa kuanzisha vita na Papa.
Karibu 60% ya Wakatoliki Wazungu wanaunga mkono jinsi Trump anavyoshughulikia uhamiaji, kulingana na utafiti mpya uliofanywa na taasisi ya Public Religion Research Institute.
Nguvu na umaarufu wa Wakatoliki wa mrengo wa kulia katika nyanja ya kisiasa, zinaongozwa na JD Vance, ambaye anasema siasa zake zinaundwa na imani yake.
Amesema sera ya sasa juu ya uhamiaji haipingani na mafundisho ya Kanisa, pia amesema kuna jukumu la kukumbuka ubinadamu kwa watu walio nchini kinyume cha sheria.
Lakini baadhi ya Wakatoliki kama Jeanne Rattenbury wa Kanisa Katoliki la St Gertrude huko Chicago, jiji ambalo ni kitovu cha utekelezwaji wa sheria za uhamiaji za utawala wa Trump, anasema:
“Ninajivunia kuwa Mkatoliki kuanzia Kanisa Katoliki, Papa hadi maaskofu, wahamiaji wana haki ya kutendewa kwa heshima. Wana haki ya kuheshimiwa utu wao.”
Ingawa Wakatoliki wengi wa Marekani wanashikilia misimamo ya kihafidhina kuhusu masuala kama vile utoaji mimba, sawa na msimamo wa Kanisa. Lakini karibu theluthi moja ya Wakatoliki Wazungu kwa upande mwingine hupigia kura Chama cha Democratic mara kwa mara.
Na karibu theluthi moja ya Wakatoliki nchini Marekani walizaliwa katika nchi zingine. “Hili ni kanisa lililojengwa juu ya uhamiaji,” anasema David Gibson.
‘Haiendani na Injili’
Chanzo cha picha, Getty Images
Askofu Joseph Tyson wa Yakima, Jimbo la Washington, alikuwa mmoja wa watu 216 waliounga mkono Ujumbe wa USCCB. Maaskofu watano pekee walipiga kura ya kupinga na watatu walijizuia.
“Kuna kutokukubaliana kuhusu jinsi kanisa linavyowaona wahamiaji, kutokana na jinsi utawala wa sasa unavyowaona wahamiaji.”
“Tunaona mambo mengi chanya katika wahamiaji hao.”
Anasema hatetei mipaka kuachwa wazi, jambo ambalo Papa Leo pia amelisema, lakini anapinga “kufukuzwa bila mpangilio.”
“Uhamishaji tunaouona wa waumini wetu na watu wetu nchini Marekani sio wenye ufanisi au kuwalenga wahalifu,” anasema askofu.
Anakadiria kwamba karibu nusu ya familia katika dayosisi yake yenye wakazi wengi wenye asili ya Kihispania zina mtu katika familia yao anayekabiliwa na aina fulani ya tatizo kuhusu hadhi yao ya uhamiaji. Mapadre pia mara nyingi ni wahamiaji wenyewe, na hivyo kuliweka Kanisa katika hali ngumu zaidi.
“Mtu yeyote anaweza kunyang’anywa makaratasi yake, [kwa hivyo] tuna watu wetu wanaobeba makaratasi wakati wote.”
Askofu Tyson anasema sera ya sasa ya Marekani inapingana na mafundisho ya Kikatoliki.
Hata hivyo, kwa Jesse Romero, ni maaskofu wa Marekani na Papa ndio wanaopinga mafundisho ya Kikatoliki. Anasema Katekisimu iko wazi kwamba wahamiaji wanapaswa kufuata sheria zote, ikiwa ni pamoja na zile zinazohusu uhamiaji.
Romero anasema ngawa anamkubali Papa na maaskofu kama viongozi wa imani, “haimaanishi kwamba katika maoni yao binafsi, watasema kila kitu sawa. Wao ni binadamu.”
“Mtu pekee asiye na dhambi ni Yesu. Yeye ni mkamilifu. Kwa wengine, tunapaswa kuombeana.”
Imetafsiriwa an Rashid Abdallah nakuhaririwa na Ambia Hirsi