JESHI la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama limehakikishia umma kwamba linaendelea kuimarisha ulinzi wakati wote wa sherehe za mwisho na mwanzo wa mwaka, zinazotanguliwa na Krismasi itakayoadhimishwa kesho.
Hii ni taarifa njema kuona ambavyo vyombo hivi vya ulinzi na usalama vimeendelea kuwa ‘macho’ wakati wote, kwa ajili ya kulinda amani ya nchi na watu wake.
Taarifa hii ni yenye matumaini, maana polisi imesema hali ya usalama wa nchi ni shwari, kutokana na uelewa wa Watanzania juu ya umuhimu wa kila mmoja kulinda na kuimarisha amani, utulivu na usalama.
Ni habari njema zaidi kutokana na ukweli kwamba, ibada za Krismasi zinazotanguliwa na mkesha zinahitaji mazingira salama ili kila mmoja aweze kushiriki kikamilifu katika kusherehekea sikukuu hii ya kidini.
Kwa ujumla, amani ni msingi wa maisha ya kila siku na msingi wa maendeleo ya jamii. Bila amani, hata sikukuu hizi za mwanzo na mwisho wa mwaka haziwezi kusherehekewa.
Ni ukweli ulio wazi, Jeshi la Polisi linafanya kazi kwa bidii, likihakikisha hakuna uharibifu, wizi, au vurugu.
Hivyo, ni jukumu la kila Mtanzania kuunga mkono juhudi hizi kwa dumisha hali ya amani bila kuachia jeshi
hilo pekee. Ushirikiano wa wananchi na vyombo vya ulinzi na usalama ni muhimu.
Kila mwananchi ana nafasi ya kuonesha uwajibikaji wake kwa kuchukua hatua za kuzuia vurugu, kumwambia
mwenzake asiingie kwenye tabia za fujo na kuepuka kuzidisha hali zinazoweza kusababisha migogoro.
Ifahamike wazi kwamba, hakuna ibada inayoweza kufanyika kwa utulivu ikiwemo mkesha wa Krismasi, endapo
kutakuwa na uhalifu na vurugu.
Kwa hiyo, ni muhimu na wajibu wa kila mtu kwa nafasi yake kudhibiti viashiria vya vurugu au tabia hatarishi ili kutoruhusu watu wa namna hiyo kuharibu furaha ya walio wengi.
Hii ni nafasi ya wananchi kuendelea kuonesha mshikamano katika kupambana na yeyote mwenye dhamira ya kuharibu amani ya nchi na watu wake.
Siku hizi za furaha zisitumiwe kuwa kivutio cha fujo, bali fursa ya kuimarisha uhusiano, kushirikiana na kuthamini utulivu unaowezesha kila mmoja kufurahia sikukuu.
Kwa kuendelea kudumisha amani kwa vitendo, ni wazi Krismasi na Mwaka Mpya vitaadhimishwa kwa furaha
halisi, heshima na kudumisha mshikamano wa kitaifa.
Hima Watanzania, amani si mali ya mtu mmoja bali ni urithi wa kila mmoja. Amani ni kila kitu. Tuilinde, tuithamini na tuidumishe.
