
Waziri wa Vita wa Israel amelazimika kufuta matamshi yake saa chache tu baada ya kudai kuwa kamwe utawala wa Kizayuni hautaondoa wanajeshi wake vamizi kwenye Ukanda wa Ghaza.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Mehr, waziri wa vita wa Israel, Israel Katz amefuta haraka madai yake ya awali kwamba jeshi la utawala huo litabakia milele kwenye Ukanda wa Ghaza na amesisitiza kwamba baraza la mawaziri la Tel Aviv halina nia ya kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ukanda huo.
Kulegeza kamba waziri wa vita wa Israel baada ya kudai kuwa wameamua kuikalia kwa mabavu moja kwa moja Ghaza, kumekuja saa chache tu baada ya kutoa matamshi hayo wakati wa sherehe ya kusaini makubaliano ya kujenga vitongoji vipya 1,200 vya walowezi wa Kizayuni katika eneo la Beit El linalokaliwa na Wazayuni karibu na Ramallah, Ukingo wa Magahribi wa Mto Jordan.
Duru za habari za Israel zimedai kwamba mashinikizo ya Marekani ndiyo yaliyomlazimisha waziri wa vita wa Israel kufuta haraka matamshi yake hayo.
Ikumbukwe kuwa baada ya kutolewa matamshi hayo, afisa wa Marekani aliyeko kusini mwa maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu na Wazayuni ambayo yamepachikwa jina bandia la Israek kudai kwamba Wamarekani wamekasirika waliposikia matamshi ya Katz na wameona yanapingana na mpango wa Trump kuhusu Ukanda wa Ghaza.
Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, huenda matamshi ya waziri wa vita wa Israel ya kubakia milele kwenye Ukanda wa Ghaza ndio uhalisia wa mambo isipokuwa tu Katz ameyatoa kabla ya kufika muda wake.
Waziri wa Vita wa Israel amedai pia kwamba: Tel Aviv kamwe haitoondoa wanajeshi wake Ukanda wa Ghaza bali itajenga vitongoji vya waloweizi wa Kizayuni kaskazini mwa ukanda huo.