
Neno “G20” lilikuwa ndilo neno lililotumika mara nyingi zaidi nchini Afrika Kusini mwaka wa 2025. Hayo ni kwa mujibu wa Bodi ya Lugha ya Afrika Kusini (PanSALB).
Bodi ya PanSALB imesema katika taarifa yake ya Jumanne kwamba imefanya utafiti wa kina na kuchunguza kwa kushirikiana na shirika la utafiti wa vyombo vya habari la Focal Points na kuchambua data mbalimbali na mwishowe imegundua kuwa neno “G20” ndilo lililotumiwa zaidi na vyombo vya habari vyenye itibari, vya uchapishaji, utangazaji na mitandaoni, katika mwaka huu unaokaribia kuisha wa 2025 na kwa mujibu wa bodi hiyo, neno hilo ndilo maarufu zaidi Afrika Kusini hivi sasa. Kwa mujibu wa bodi hiyo ya PanSALB, mchakato wa kuteua maneno ulihusisha maneno hayo kwa mujibu wa matumizi halisi ya lugha.
“G20” iliibuka kama neno kuu lililotajwa na kuznugmzia zaidi nchini Afrika Kusini kutokana na nchi hiyo kuwa mwenyeji wa kikao cha wakuu wa kundi la nchi tariri zaidi duniani cha G20 kwa mwaka huu wa 2025. Ikumbukwe kuwa Marekani kwa amri ya Donald Trump ilisusia kikao hicho kwa kudhani kwamba ingeliweza kupunguza umaarufu wake, lakini ilishindwa.
Maneno “Serikali ya Umoja wa Kitaifa” na “Ushuru” yalishika nafasi ya pili na ya tatu, mtawalia, ikiwa ni udhibitisho wa kuweko maendeleo muhimu ya kisiasa, ushiriki wa kimataifa na mijadala ya kijamii na kiuchumi nchini Afrika Kusini.
PanSALB ni bodi iliyopewa jukumu la kukuza lugha nyingi, yaani kukuza na kuhifadhi lugha 12 rasmi za Afrika Kusini, na kulinda haki za lugha hizo. Lugha rasmi za Afrika Kusini ni Ndebele, Pedi, Sotho, Sign, Swazi, Tsonga, Tswana, Venda, Afrikaans, Xhosa, Zulu na Kiingereza.