Kundi la wabunge 150 wa Iran limeilaani vikali Marekani kwa chokochoko zake huko Venezuala na kuzuia meli za mafuta katika Bahari ya Karibi, likisema kuwa vitendo hivyo vya Washington ni uharamia wa baharini na ni tishio kwa utulivu na usalama wa ukanda huo.

Kwenye taarifa yao ya pamoja iliyosomwa leo Jumatano bungeni na Mojtaba Bakhshipour ambaye ni mjumbe wa bodi inayoongoza bunge la Iran, wabunge hao wamesema kuwa, kuzuiwa na kutekwa nyara meli za mafuta na za kibiashara pamoja na kuongezeka chokochoko za kijeshi za Marekani dhidi ya Venezuela ni mbinu za kiwoga ambazo zinakanyaga sheria za kimataifa.

Wabunge hao wa Iran wameonya kwamba, uwepo mkubwa wa kijeshi wa Marekani katika eneo la Karibi unadhoofisha usalama wa ukanda huo, na unaonesha kupuuza waziwazi Washington, uhuru wa mataifa mengine.

Wameilaumu Washington kikamilifu kwa kusababsiha mivutano na kuhatarisha amani na utulivu wa eneo la Karibi wakisisitiza kwamba vitendo vya Marekani vinatishia kuutumbukiza ukanda huo katika vita na mapambano makali zaidi.

Taarifa hiyo ya Wabunge 150 wa Iran pia imetangaza mshikamano wao na serikali ya Venezuela na watu wake, ikitoa mwito wa kukomeshwa mara moja vitisho, vikwazo na mashinikizo ya Marekani dhidi ya Caracas.

Kwa upande wake, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran nayo imetoa taarifa kali ikilaani vitisho vya Marekani vya kuiwekea Venezuela kizuizi cha baharini kwa upande mmoja.

Katika miezi ya hivi karibuni, Marekani imeongeza mashinikizo yake dhidi ya Venezuela kupitia kupeleka kundi kubwa la wanajeshi katika eneo la Karibi kwa madai yasiyo na ushahidi wowote ya maafisa wa Marekani kwama eti eneo hilo linatumiwa na baadhi ya watu kusafirisha dawa za kulevya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *