
ZAIDI ya wananchi 700 kutoka kaya 234 katika vijiji vitano vya wilaya ya Pangani, mkoani Tanga, wanatarajiwa kulipwa fidia ya Sh bilioni 35 kupisha utekelezaji wa mradi wa mchanga mzito (Madini ya Tembo).
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Mzambarauni, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk. Batilda Burian, aliwataka wananchi kuendelea kuwa watulivu wakati serikali ikiendelea na zoezi la uthamini. “Niwaombe wananchi muendelee kuwa watulivu wakati huu ambapo mthamini mkuu wa serikali anaendelea na uhakiki wa tathmini kabla ya wananchi kulipwa fidia zao,” alisema Dk. Burian.

Aliongeza kuwa ofisi yake inaendelea kufuatilia kwa karibu zoezi hilo kuhakikisha wananchi wote waliopisha maeneo yao wanalipwa fidia stahiki kama ilivyoainishwa kisheria. Kwa upande wake, Mhandisi Heri Issa Gombero kutoka Kampuni ya Nyati inayosimamia mradi huo, alisema miradi hiyo inahusisha vijiji vya Stahabu, Bweni, Mzambarauni, Mikinguni na Mwera. SOMA: Mradi kutoa uhakika wa maji saa 24 Tanga