TANGA: Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Tanga (TangaUWASA) imesema mradi wa hatifungani ya kijani unatarajiwa kukamilika Machi 2026.

Mradi huo utawapa wakazi wa mkoa huo uhakika  wa majisafi na salama kwa masaa 24 katika maeneo ya kihuduma ya Jiji la Tanga pamoja na miji ya Muheza, Pangani, na Mkinga.

Mkurugenzi wa Usambazaji Maji, Mhandisi Salum Ngumbi, ametoa hakikisho hilo wakati wa ziara ya waandishi wa habari mkoani humo ya kutembelea na kujionea hatua mbalimbali za maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa hatifungani pamoja na kupata taarifa ya hali ya huduma.

Amesema kuwa mradi huo utaongeza kiwango cha uzalishaji na usambazaji wa maji kutoka mita za ujazo 45,000 hadi mita za ujazo 60,000 kupitia uboreshaji wa miundombinu ya usambazaji maji kwa kulaza mabomba makubwa yenye kipenyo cha mm 600.

Pia upanuzi wa kituo cha kusafisha maji na kutibu maji cha Mowe, ujenzi wa tanki la kuhifadhia maji lenye ukubwa wa mita za ujazo 35,000 sambamba na kuimarisha shughuli za utunzaji na uhifadhi wa vyanzo vya maji na kwa sasa mradi umefikia asilimia 45 ya utekelezaji wake.

Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TangaUWASA, Dk Fungo Ali Fungo amesema kuwa katika mwaka huu Mamlaka imeendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji kwa lengo la kuendelea kuimarisha na kuboresha hali ya upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi.

“Tunawashukuru sana kwa ushirikiano mnaoendelea kutuonesha katika kufanikisha upatikanaji wa huduma bora na ya uhakika kwa wananchi pamoja na kutambua jitihada za taasisi, ambapo kwa mwaka huu tumekuwa na miradi kadhaa ya thamani kubwa kwa mdhumuni ya kuhakikisha kuwa huduma zinawafikia wananchi na utekelezaji wa miradi husika inaendelea kwa kasi kama ambavyo tumeshuhudia na tutahakikisha kuwa tunakamilisha kwa wakati uliopangwa,” amesema Dk Fungo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *