Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier amewahimiza wajerumani waoneshe ujasiri, hali ya kujiamini na amesisitiza mwito wa kuendeleza mshikamano na Ukraine. Steinmeier ameyasema hayo katika hotuba yake ya kuadhimisha Krismasi. Pia ametoa mwito wa mdahalo wa wazi na kuzingatiwa kwa maadili ya Kiulaya.

Kiongozi huyo wa Ujerumani amesema wajerumani wanapaswa kuwa na ujasiri wa kuwapa nguvu ya kuanza upya katika mambo yote makubwa na madogo ambayo watu wanakusudia kuyafanya kwa kutegemea uwezo wa kila mtu.

Ujerumani Bonn 2025 | Soko la Krismasi mjini Bonn
Soko la Krismasi mjini BonnPicha: Ying Tang/NurPhoto/picture alliance

Ameeleza kuwa mambo kadhaa yanasababisha kiza katika maisha ya binadamu kama vile migogoro, vita na mikosi ya kupoteza ajira. Hata hivyo Rais Frank-Walter Steinmeir amesema matumaini bado yapo katika jamii, familia na katika jumuiya za kuwaleta watu pamoja.

Katika hotuba yake Steinmeier amesisitiza umuhimu wa kusherehekea Krisimasi inayoleta faraja, matumaini na hali ya uhakika miongoni mwa watu.

Kiongozi huyo wa Ujerumani ameeleza kuwa uhakika huo unawapa wajerumani imani ya kuweza kujenga nguvu na hivyo kujizatiti katika kuyatekeleza majukumu ya kuijenga dunia bora na kuwatumikia binadamu wenzetu.      

Pamoja na hayo Steinmeier amehimiza juhudi za kuendeleza midahalo ya  wazi. Amesea ikiwa wajerumani watafanya juhudi za pamoja za kutafuta mwelekeo na malengo, watapata mafanikio makubwa. Rais wa Ujerumani pia ameshauri umuhimu wa kuwapa wengine fursa ya kutoa maoni yao badala ya kuwasakama na kile ambacho wengine wanakiona kuwa ni sahihi.

Ujerumani Berlin 2025 | Rais Frank-Walter Steinmeier alipomkaribisha Rais Volodymir Zelensky
Kushoto Rais wa Ukraine Volodymir Zelensky. Kulia: Rais wa Ujerumani Frank-Walter SteinmeierPicha: Maryam Majd/AP Photo/picture alliance

Katika hotuba yake kiongozi huyo wa Ujerumani pia amesisitiza umuhimu wa kuendeleza mshikamano na watu wa Ukraine wanaopambana na uvamizi wa Urusi. Pia ametilia maanani juhudi zinazofanywa kwa lengo la kuleta amani. Amesisitiza kwamba juhudi hizo zinaleta matumaini.

Rais wa Ujerumani pia amehimiza umuhimu wa kuyazingatia maadili ya Kiulaya yaani, amani, demokrasia, uhuru na hadhi ya binadamu ambayo amesema asilani hayataachwa na watu wa Ulaya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *