Dar es Salaam. Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Dar es Salaam, Taddeus Ruwa’ichi, ametangaza kuugua kwa Askofu Mkuu mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo (81) na kwamba atasafirishwa kupelekwa nje ya nchi kwa matibabu.

Taarifa iliyotolewa leo, Jumatano Desemba 24, 2025, na kutiwa saini na Askofu Ruwa’ichi na Kansela Vincent Mpwaji, inaeleza kwamba Kardinali Pengo atapelekwa nchini India kwa ajili ya matibabu.

Hatua hiyo, kwa mujibu wa taarifa hiyo, ni baada ya kiongozi huyo wa kiroho kukabiliwa na changamoto za afya kwa kipindi fulani, na kwamba imepangwa matibabu yake yafanyike nje.

“Zimefanyika jitihada za kumsaidia kimatibabu hapa kwetu, imeonekana kwamba upo uhitaji wa kumpeleka nje ili apate matibabu ya uhakika zaidi,” imeeleza taarifa hiyo.

Imesema mipango imefanyika ili akatibiwe nchini India na kwamba inatarajiwa ataondoka siku za karibuni.

“Nawaalika nyote tuungane kumsindikiza kwa sala na matashi mema,” imeeleza taarifa hiyo.

Kadinali Pengo ni nani?

Kardinali Pengo alizaliwa Agosti 5, mwaka 1944, na sasa ametimiza umri wa miaka 81. Amekuwa Kadinali wa pili nchini Tanzania, baada ya Laurean Rugambwa.

Kwa mara ya kwanza, Novemba mwaka 1983, Papa Yohane Paulo II alimteua kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Nachingwea, mkoani Lindi.

Mwaka 2022, alisherehekea miaka 38 ya uaskofu, pia ilikuwa maadhimisho ya Jubilei ya miaka 50 tangu alipopewa Daraja Takatifu ya Upadri, na ukawa ni mwanzo wa kurasa za maisha yake kama Askofu na hatimaye Kardinali.

Kardinali Pengo ndiye aliyekuwa Padri wa kwanza Mtanzania kuwekwa wakfu kuwa Askofu na Mtakatifu Yohane Paulo II kwa ajili ya kuwafundisha na kuwaongoza Watanzania.

Kiongozi huyo wa kiroho aliyezaliwa Sumbawanga, mkoani Rukwa, baada ya masomo na mafunzo yake ya kikasisi, Juni mwaka 1971 alipewa daraja la upadri.

Kwa kipindi cha miaka miwili, yaani kuanzia mwaka 1971 hadi mwaka 1973, aliteuliwa kuwa Katibu wa Askofu wa Jimbo Katoliki la Sumbawanga.

Kati ya mwaka 1973 hadi mwaka 1977, alitumwa na Jimbo Katoliki la Sumbawanga kuendelea na masomo ya juu kwenye Chuo Kikuu cha Kipapa la Lateran, Kitivo cha Taalimungu Maadili cha Alfonsianum, kilichoko mjini Roma.

Aliporejea nchini baada ya kuhitimu masomo yake, alitumwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kwenda kufundisha maadili katika Seminari Kuu ya Kipalapala, iliyoko Jimbo Kuu la Tabora.

Kuanzia mwaka 1978 hadi 1983, aliteuliwa na TEC kuwa muasisi wa Seminari Kuu ya Segerea, iliyoko Jimbo Kuu la Dar es Salaam.

Novemba mwaka 1983, aliteuliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Nachingwea, na Oktoba 17, 1986, akatangazwa kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Tunduru-Masasi.

Baadaye, Januari 1990, Mtakatifu Paulo II akamteuwa kuwa Askofu Mkuu Mwandamizi mwenye haki ya kurithi Jimbo Kuu la Dar es Salaam, na kuingia jimboni Mei 24, 1990.

Februari 12, 1992, akasimikwa kuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, na Februari 21, akateuliwa na Mtakatifu Paulo II kuwa Kardinali.

Hatua hiyo, imaifanya Tanzania kuweka historia ya kupata Kardinali mpya miezi michache baada ya kufariki dunia Kardinali Laurean Rugambwa.

Kati ya mwaka 2007 hadi 2009, alichaguliwa kuwa Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar (SECAM).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *