Muungano wa Nchi za Sahel (AES) unaendelea kuchukua hatua mpya kuelekea kujitegemea kikanda, huku viongozi wa kijeshi wa Mali, Niger na Burkina Faso wakifanya mazungumzo mjini Bamako huku wakizindua televisheni yao ili kuwawezesha kukanusha upotoshaji.

Awamu ya pili ya mkutano wa kilele wa AES umelenga kuimarisha ushirikiano ndani ya muungano huo na kupunguza utegemezi kwa jumuiya ya kikanda ya Afrika Magharibi (Ecowas).

Mkutano huo umejikita katika masuala ya ulinzi na usalama, maendeleo, mawasiliano, pamoja na juhudi za kupambana na ugaidi katika nchi hizo tatu.

Rais wa Mali, Assimi Goïta, na Rais wa Niger, Abdourahamane Tchiani, walikutana katika uwanja wa ndege wa Bamako Jumatatu kabla ya kuelekea katika Ikulu ya Rais.

Rais wa Burkina Faso, Ibrahim Traoré, alijiunga na mkutano huo jana Jumanne Desemba 23, 2025 asubuhi na ni miongoni mwa wanaotajwa kuweza kushika kijiti kuongoza umoja huo kwa awamu nyingine.

Mali, Niger na Burkina Faso ziliunda muungano huo mwaka 2023 na kujiondoa rasmi kutoka ECOWAS mwaka jana.

Hatua hiyo ilitokana na mvutano kati ya nchi hizo tatu na washirika wao wa Magharibi baada ya mapinduzi ya kijeshi.

Kabla ya mkutano huo wa kilele, nchi hizo tatu zilitangaza rasmi kuundwa kwa kikosi cha pamoja cha kijeshi cha kupambana na ugaidi katika eneo hilo.

Jana Jumanne, Goïta, Tchiani na Traoré pia walizindua kituo cha televisheni cha Muungano wa Nchi za Sahel. Kituo hicho kimeelezwa kitakuwa ni chombo cha kupambana na upotoshaji wa taarifa na kukuza maslahi ya muungano huo.

Baada ya Goïta kuteuliwa kuwa rais wa muungano huo katika mkutano wa mwaka jana, inatarajiwa kuwa kiongozi mpya wa AES atatangazwa mjini Bamako wiki hii.

Ecowas imeeleza kuwa bado iko tayari kuruhusu Mali, Niger na Burkina Faso kuendelea kunufaika na baadhi ya fursa za jumuiya hiyo, ikiwemo biashara, licha ya kujiondoa kwao.

Hata hivyo, nchi hizo tatu zinazoongozwa na serikali za kijeshi zimechukua hatua za kudhihirisha kujitegemea kwao kwa kuanzisha hati zao za kusafiria kwa raia wao.

Nchi hizo tatu bado ni wanachama wa Umoja wa Kiuchumi na Kifedha wa Afrika Magharibi (Uemoa), unaohakikisha kuendelea kwa biashara na uhuru wa usafirishaji wa bidhaa miongoni mwa wanachama wake wanane, wakiwemo Senegal, Ivory Coast, Guinea-Bissau, Togo na Benin.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *