Zaidi ya wananchi 10,000 kutoka vijiji 45 katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, Mkoa wa Mbeya, wameanza kunufaika na Mradi wa Kuimarisha Mbinu za Asili za Kijamii za Usimamizi wa Mazingira na Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi (NBS–USANGU), unaolenga kulinda na kuimarisha vyanzo vya maji katika Bonde la Usangu.
Mradi huo pia unahusisha uchimbaji wa visima virefu vya maji kwa matumizi ya watu na sekta ya elimu, hatua inayolenga kuhakikisha upatikanaji wa rasilimali hiyo muhimu kwa uhakika.
Mradi una thamani ya Dola 2.8 milioni za Marekani (Zaidi ya Sh6 bilioni na unatekelezwa na Bodi ya Maji Bonde la Rufiji chini ya Wizara ya Maji, kwa ufadhili wa Benki ya Dunia kupitia serikali ya Japan.
Utekelezaji wake ni sehemu ya jitihada za Serikali kuhakikisha usimamizi endelevu wa rasilimali za maji kwa masilahi ya kijamii na kiuchumi, hususan katika maeneo yanayokabiliwa na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Mratibu wa Mradi wa Kuimarisha Mbinu za Asili na Kijamii za Usimamizi wa Mazingira na Kuhimili Mabadiliko ya Tabia Nchi (NBS-USANGU), David Muginya akitoa ufafanuzi wa utekelezaji wake. Picha na Hawa Mathias
Akizungumza leo Jumatano Desemba 24, 2025, katika kikao kazi cha tathmini ya utekelezaji wa mradi huo, Mratibu wa Mradi wa NBS–USANGU, David Muginya amesema maandalizi ya mradi yalianza kufanyiwa tathmini mwaka 2022 na kukamilika mwaka 2024, kabla ya kusainiwa rasmi na Serikali kupitia Wizara ya Fedha na kuanza kutekelezwa katika mwaka wa fedha 2025/2026.
Amesema lengo kuu la mradi ni kuimarisha usimamizi wa mazingira, kulinda vyanzo vya maji na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, hasa katika Bonde la Usangu ambalo limekuwa likikabiliwa na changamoto ya uvamizi wa vyanzo vya maji.
“Miongoni mwa mikakati tuliyojiwekea ni kuwawezesha wananchi wanaofanya shughuli ndani ya maeneo ya hifadhi ya vyanzo vya maji kupata fedha ili kuanzisha shughuli mbadala za kiuchumi na kuondoka ndani ya mita 60 za hifadhi,” amesema Muginya.
Amesema Bonde la Usangu ni eneo muhimu kwa uchumi wa Taifa, kwa sababu linachangia takribani asilimia 15 ya maji yanayoingia kwenye mabwawa makubwa ya kuzalisha umeme, yakiwemo Mtera, Kidatu na Bwawa la Mwalimu Nyerere.
Kwa mujibu wa Muginya, Bodi ya Maji Bonde la Rufiji imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kufukua mito iliyobadili mikondo yake na kuimarisha vyanzo vya maji ili kuboresha mtiririko wa maji yanayoelekea kwenye mabwawa ya kuzalisha umeme.
“Ujio wa mradi huu unalenga kuhakikisha mito na vyanzo vya maji vinalindwa na kuimarishwa ili mabwawa ya kuzalisha umeme yapate maji ya uhakika muda wote,” amesema Muginya.
Ameongeza kuwa Bonde la Usangu ni miongoni mwa maeneo yaliyoathirika zaidi na mabadiliko ya tabianchi, likipokea mvua chini ya wastani wa milimita 400 hadi 1,000 kwa mwaka, hali inayochangia ukame wa mara kwa mara licha ya kuwa eneo muhimu kwa kilimo cha mpunga.
Hata hivyo, Muginya amesema mradi huo haujajikita katika sekta ya nishati pekee, bali unalenga pia kuboresha upatikanaji wa maji kwa matumizi ya kijamii, kilimo na mifugo. Kupitia mradi huo, shughuli mbalimbali tayari zimeanza kutekelezwa ikiwemo uchimbaji wa visima virefu katika shule, zahanati na maeneo ya jamii, pamoja na ujenzi wa mabakuli ya kunyweshea mifugo kwa jamii za wafugaji zilizoathirika zaidi na mabadiliko ya tabianchi.
Kauli za wananchi
Mkazi wa Kijiji cha Igomelo, Juma Mwakasese amesema mradi huo utasaidia kupunguza migogoro ya wakulima na wafugaji iliyokuwa ikichochewa na upungufu wa maji.
“Upatikanaji wa mabakuli ya kunyweshea mifugo umeondoa tabia ya mifugo kuingia kwenye mashamba na vyanzo vya maji. Hii imerejesha amani katika jamii yetu,” amesema.
Naye Rehema Ngowi, mkazi wa kijiji cha Uturo amesema uchimbaji wa visima virefu umepunguza adha ya kutembea umbali mrefu kutafuta maji.
“Awali tulikuwa tunatembea zaidi ya kilomita tatu kutafuta maji, lakini sasa yanapatikana karibu na makazi yetu, jambo lililopunguza mzigo mkubwa kwa wanawake na watoto,” amesema.
Mfugaji Abdallah Komba wa kijiji cha Chimala amesema mradi huo umeongeza uhimilivu wa jamii ya wafugaji wakati wa kiangazi.
“Mabakuli ya kunyweshea mifugo yameokoa mifugo yetu. Hata kipindi cha kiangazi tunapata maji bila kuingia kwenye maeneo ya hifadhi,” amesema.
Akizungumzia hilo,Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Rufiji, Mhandisi David Munkyala amesema mradi huo ni miongoni mwa miradi ya kimkakati inayolenga kuhakikisha rasilimali za maji zinalindwa kwa masilahi mapana ya uchumi wa Taifa.
Amesema bodi iliandaa andiko la kuomba ufadhili kutoka Serikali ya Japan na kufanikiwa kupata fedha kupitia Benki ya Dunia, kwa lengo la kulinda rasilimali za maji kwa matumizi ya jamii, kilimo, mifugo na uzalishaji wa nishati ya umeme.
“Tumekuja na suluhisho la kujenga miundombinu ya kunyweshea mifugo ili kupunguza uvamizi wa vyanzo vya maji, ambao umekuwa changamoto kubwa katika bonde hili,” amesema.
Ameongeza kuwa mradi huo umeanza kutekelezwa katika mwaka huu wa fedha na unatarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha miaka mitatu, huku wananchi zaidi ya 10,000 wakitarajiwa kunufaika moja kwa moja.