Kampuni ya Mawasiliano Yas, imekuwa miongoni mwa wadhamini wa Rombo Marathon 2025, tukio lililoleta wanamichezo kutoka Tanzania na nje ya nchi pamoja, likilenga kuhamasisha michezo, mshikamano wa kijamii, na utunzaji wa mazingira.
Mgeni rasmi wa hafla ya kufunga mbio hizo, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, aliwashukuru wadhamini, ikiwemo kampuni hio, kwa kuunga mkono jitihada za kukuza michezo na maendeleo ya jamii.
“Mbio hizi za Rombo Marathoni zinaonyesha kuwa michezo si tu burudani, bali pia ni chachu ya maendeleo, mshikamano wa kijamii, na fursa ya utalii. Tumewapokea wageni kutoka nchi mbalimbali, na tunatarajia mwakani mbio hizi ziwe bora zaidi,” alisema Babu.
Mbunge wa Rombo na mlezi wa mbio hizo, Adolf Mkenda, aliishukuru Yas kwa udhamini wake na kuashiria matarajio makubwa kwa maendeleo ya mashindano haya.
“Kushiriki katika Rombo Marathoni kunaleta faida nyingi kwa kila mshiriki. Mbio hizi zinahamasisha afya, mshikamano wa kijamii, na pia zinasaidia kutangaza Rombo na Kilimanjaro kote Tanzania na kimataifa,” alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Yas Kanda ya Kaskazini, Ndugu Henry Kinabo, alisema kuwa,
“Yas inaamini michezo ni sehemu muhimu ya kuimarisha afya, mshikamano wa kijamii, na kukuza uchumi. Rombo Marathon ni fursa ya kipekee kuonyesha uzuri wa Rombo, mkoa wa Kilimanjaro, na Tanzania kwa ujumla,” alisema Ndugu Kinabo.
Aidha, alibainisha kuwa mbio hizi pia ni fursa ya kuhamasisha utunzaji wa mazingira, ikizingatiwa kwamba ardhi, vyanzo vya maji, na uoto wa asili katika maeneo haya ni rasilimali muhimu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
“Rombo Marathon inatukumbusha wajibu wetu wa kulinda ardhi, vyanzo vya maji, na uoto wa asili unaozunguka mji na vijiji vyetu,” alisema.
Ndugu Kinabo pia aliongeza kuwa Yas inaendelea kuwekeza katika miundombinu ya mawasiliano, ikiwemo upatikanaji wa mtandao wa 4G katika maeneo yote na 5G katika miji, ili kurahisisha mawasiliano, biashara, na elimu kwa wakazi wa Kanda ya Kaskazini.
Kampuni ya Yas imesisitiza dhamira yake ya kushirikiana na waandaaji wa Rombo Marathon kuhakikisha mashindano haya yanaendelea kukua, kuboresha viwango, na kuvutia washiriki wengi zaidi kutoka ndani na nje ya Tanzania.