Dar es Salaam. Watu wanane wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na shtaka moja la kusafirisha dawa za kulevya aina ya bangi zenye uzito wa kilo 90.89.

Wakili wa Serikali, Tumaini Mafuru amewataja majina washtakiwa kuwa ni  Jaribu Tindwa, Juma  Mfumo, Rahim Nampanda, Aboubakari Ally, Nurdin Mussa(36), Farid Rashid(36), Ally Neesha na Mussa Kipande (38).

Washtakiwa hao wamefikishwa mahakamani hapo leo Jumatano Desemba 24, 2025 na kusomewa mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Rahim Mushi.

Akiwasomea mashtaka yao, wakili Mafuru alidai washtakiwa wanadaiwa Novemba 2, 2025 eneo la Malamba Mawili lililopo eneo la Mbezi wilayani Ubungo Dar es Salaam, washtakiwa hao walikutwa wakisafirisha dawa za kulevya aina ya bangi zenye uzito wa kilo 90.89.

Washtakiwa hao wanadaiwa kuwa dawa hizo walizisafirisha kutoka Lilongwe nchini Malawi na kuja nazo nchini.

Washtakiwa baada ya kusomewa kesi hiyo, upande wa Jamhuri ulidai kuwa upelelezi wa kesi bado haujakamilika, hivyo wapangiwe tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa na kuangalia iwapo upelelezi wa kesi hiyo umekamilika au laa.

Hakimu Mushi aliahirisha kesi hiyo hadi  Januari 7, 2025 kwa ajili ya kutajwa na washtakiwa wote walirudishwa rumande.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *