Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI) Prof. Riziki Shemdoe ameulekeza uongozi wa Shirika la Masoko kuhakikisha zoezi la upangishaji wa vizimba na vyumba kwa wafanyabishara wa Soko la Kariakoo uzingatie bei ya soko ili mradi huo wa Soko la Kariakoo uwanufaishe wafanyabiashara kama ilivyokusudiwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Prof. Shemdoe ametoa maelekezo hayo wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua maendeleo ya ukarabati wa soko, ambao ulianza kutekelezwa Januari 7, 2022 na kukabidhiwa katika Shirika la Masoko ya Karikakoo Agosti 25, 2025.
“Mpangishe vizimba na vyumba kwa kuzingatia bei ya soko kwani Mhe. Rais alitoa Shilingi Bilioni 28 za ukarabati wa soko ili wafanyabishara wanufaike, hivyo kusiwe na ujanja ujanja wa baadhi ya watu kufanya udalali,” Prof. Shemdoe.
Sanjari na hilo, Prof. Shemdoe ameusisitiza uongozi wa Soko la Kariakoo kuwapa kipaumbele wafanyabishara wa awali wanapewa kipaumbele kupewa vizimba na vyumba kabla ya kuwapatia wafanyabiashara wapya, ili kuondokana na malalamiko.
Aidha, Prof. Shemdoe ameuhimiza uongozi wa Kariakoo kuhakikisha majengo ya Soko la Kariakoo yanakatiwa bima, na kuendelea kutoa elimu ya umuhimu wa bima kwa wafanyabiashara ili nao wakate bima kwa ajili ya kulinda mitaji yao pindi wanapokabiliana na changamoto zitakazoweza kuwarudisha nyuma kibiashara.
Prof. Shemdoe ameongeza kuwa, ujenzi wa Soko la Kariakoo umeongeza chachu kwa sekta binafsi kufanya uwekezaji katika kujenga majengo ya kibiashara kulizunguka soko hilo, hivyo amewapongeza na kuwahimiza kukamilisha majengo hao ili kuimarisha sekta ya biashara na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Tawala Msaidizi (Miundombinu), Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mhandisi Aman Mafuru amesema kuwa, ukarabati wa soko la Karikaoo umezingatia uwekaji wa miundombinu mbalimbali ikiwemo mifumo imara ya kukabiliana na ajali za moto, lifti za kubeba bidhaa, wafanyabiashara na wanunuzi wa bidhaa.