
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepitisha kwa kauli moja azimio la kuongeza muda wa Ujumbe wa Umoja wa Afrika wa Msaada na Kuweka utulivu nchini Somalia (AUSSOM) kwa mwaka mmoja zaidi, hadi tarehe 31 Desemba 2026.
Akilihutubia Baraza hilo la Usalama, Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa China katika Umoja wa Mataifa, Sun Lei, amesema pengo la ufadhili linaloikabili AUSSOM kwa sasa haliwezi kuhimilika, huku upungufu wa fedha unaoikabili Ofisi ya Umoja wa Mataifa Somalia, UNSOS, ukiibua wasiwasi. Amesema China inazitaka nchi washirika wa kimataifa, hususan wafadhili wa jadi, kutimiza ahadi zao za awali na kuchukua hatua za haraka kupunguza shinikizo la kifedha linaloikabili AUSSOM.
Kwa upande wake, Balozi wa Marekani, Jeffrey Bartos, amesema Marekani inaendelea kuonesha kutoridhishwa na baadhi ya wajumbe wa Baraza kutumia mchakato wa kuongeza muda wa dhamana kusukuma lugha inayokengeusha mjadala, ikiwemo kuhusu masuala ya kijinsia.
Wakati huo huo, Ujumbe wa Umoja wa Afrika wa Kusaidia na Kus stabilisha Somalia (AUSSOM) umepokea kwa furaha uamuzi wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wa kuongeza muda wa jukumu lake kwa mwaka mmoja zaidi.
Balozi El Hadji Ibrahima Diene, Mwakilishi Maalum wa Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika kwa Somalia na Mkuu wa AUSSOM, alieleza kuwa kuongeza muda huo ni uthibitisho wa imani ya Baraza katika nafasi ya Umoja wa Afrika ya kuendeleza amani, usalama na uthabiti nchini Somalia.