KOCHA mkuu mpya wa Simba, Steve Barker yupo katika mapumziko ya sikukuu ya Krismasi na familia yake, lakini mara ya baada ya mapumziko hayo anatarajiwa kuingia nchini wikiendi hii tayari kuanza rasmi kazi ya kuinoa timu hiyo, huku akija na majembe manne ya kumpiga tafu klabuni.

Moja ya mashine hizo zitakazotua na Barker aliyekuwa akiinoa Stellenbosch ya Afrika Kusini ni mdogo wa kocha wa zamani wa Simba, Fadlu Davids aliyepo kwa sasa Raja Casablanca ya Morocco.

Simba ilimtangaza na kumtambilisha kocha huyo Desemba 19 ili kuchukua nafasi ya Dimitar Pantev aliyesitishiwa mkataba Desemba 2, 2025 kwa makubaliano ya pande mbili na inadai-wa atatua nchini kabla ya Jumapili hii ili kuanza kazi na kikosi hicho kupitia michuano ya Kombe la Mapinduzi 2026.

Mwanaspoti limezinasa habari za ndani kuwa, Barker atakuja na wasaidizi wanne akiwamo kocha msaidizi anatayepiga kazi sambamba na mzawa Seleman Matola, kocha wa viungo, mchambuzi wa video na kocha wa makipa.

Chanzo cha ndani kutoka Simba kimeliambia Mwanaspoti, kwa kocha msaidizi anayekuja kusaidiana na Matola chini ya Barker ni Maahier Davids ambaye ni mdogo wa Fadlu Davids ambaye atakuwa msaidizi namba moja na Matola atakuwa msaidizi namba mbili katika ben-chi hilo jipya la Msimbazi.

“Kocha msaidizi namba moja ambaye anakuja naye Barker anaitwa Maahier Davids, huyu ni kocha ambaye jina lake lilipita mapema kabla ya kocha mkuu kutajwa kwa sababu mpango wa kwanza Seleman Matola akabidhiwe timu halafu msaidizi awe huyo,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;

“Lakini baada ya Barker kutambulishwa, alifanya mazungumzo na uongozi na kukubaliana atatua na benchi hilo jipya la ufundi ambalo atafanya nalo kazi kwa ukaribu na uongozi umekubaliana na pendekezo hilo, hivyo muda wowote makocha hao wote watatua nchini tayari  kuanza kazi.”

Chanzo hicho kimeendelea kwa kusema: “Ninachoweza kukwambia ni kwamba makocha wanaokuja ni wa hizo nafasi kwani zipo wazi kwa sasa. Mchambuzi wa video hakuwapo tan-gu aliyekuwepo kuondoka na Fadlu.

“Kwa upande wa kocha wa makipa aliyekuwapo awali chini ya meneja Dimitar Pantev naye ameondoka, lakini eneo la kocha wa viungo tunaongeza nguvu kwani hivi sasa tunaye kocha Xavi (Mohammed Mrishona), lakini ana majukumu ya timu ya taifa,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;.

“Makocha hao watawahi mapema kabla ya timu kuingia kambini wikiendi hii ili kuanza kazi haraka kabla ya kuanza mechi zetu za kimataifa mapema mwakani.”

Simba inayoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa Kundi D pamoja na Esperance ya Tunisia, Petro Atletico ya Angola na Stade Malien, ni moja ya timu 10 zilizotajwa kuwapo katika Kombe la Mapinduzi 2026 linalonza Des 28 Zanzibar ikipangwa Kundi  B.

Katika kundi hilo wapo pamoja na Fufuni na Muembe Makumbi itakayoanza nayo Januari 3 kisha kumalizana na Fufuni siku mbili baadae na inadaiwa kocha Barker ataitumia michuano hiyo kukisoma kikosi hicho kabla ya kufanya uamuzi ya usajili kupitia dirisha dogo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *