Watu wenye silaha wamewateka nyara wasafiri 28 Waislamu katikati ya Nigeria, mamlaka zimeripoti, likiwa ni tukio jipya katika wimbi la utekaji nyara linalotikisa taifa hilo lenye idadi kubwa zaidi ya watu barani Afrika.

Wasafiri hao, akiwemo wanawake na watoto, waliviziwa usiku wa Jumapili, wakati basi lao lilipokuwa njiani likielekea kijiji cha Gaji, eneo la utawala wa Wase katika jimbo la Plateau, kwa mujibu wa taarifa ya polisi. Vyombo vya habari vya ndani viliripoti Jumatano kuwa kundi hilo lilikuwa safarini kuelekea kwenye mkusanyiko wa kila mwaka wa Kiislamu liliposhambuliwa na wapiganaji hao.

Msemaji wa Polisi wa Jimbo la Plateau, Alabo Alfred, amesema: “Juhudi zinaendelea ili kuwaokoa waathirika na kuwatia mbaroni wahalifu.” Ameongeza kuwa kikosi maalumu cha upelelezi kimetumwa haraka eneo la tukio.

Kanda ya Kaskazini na Ukanda wa Kati wa Nigeria umekuwa ukisumbuliwa kwa miaka mingi na utekaji nyara, uporaji wa majambazi na ghasia za kijamii, huku magenge yenye silaha yakilenga mara kwa mara wasafiri, vijiji na shule.

Utekaji nyara huo ulitokea siku moja baada ya Rais wa Nigeria kutangaza kuachiliwa huru kundi la mwisho la zaidi ya wanafunzi 300 wa shule ya bweni ya Kikatoliki ya Mtakatifu Mary’s, Papiri, jimbo la Niger, waliokuwa wametekwa nyara tarehe 21 Novemba. Siku chache kabla, wasichana 25 wa shule ya bweni walitekwa jimboni Kebbi, huku wafanyakazi wawili wakipoteza maisha. Wiki moja kabla ya hapo, watu wawili waliuawa wakati kanisa moja huko Eruku, jimbo la Kwara, liliposhambuliwa; maafisa wa eneo hilo walisema waumini 38 waliotekwa katika shambulio hilo tayari wameokolewa. Aidha, watu 13 walitekwa katika shambulio jingine la kanisa jimboni Kogi tarehe 14 Desemba.

Machafuko haya yamevutia macho ya dunia, huku Rais wa Marekani Donald Trump akitishia kutuma wanajeshi nchini humo kupambana na makundi ya kigaidi kama Boko Haram, akidai makundi hayo yanawalenga tu Wakristo.

Serikali ya Nigeria imepinga madai kuwa Wakristo pekee ndio walengwa, ikisisitiza kuwa hali ya usalama inawaathiri watu wa dini zote. Mwishoni mwa mwezi uliopita, Rais Bola Tinubu alitangaza hali ya dharura ya kitaifa kuhusu usalama na kuamuru kuongezwa kwa vikosi vya jeshi na polisi kukabiliana na janga hilo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *