Harakati ya Kiislamu (Muqawama) ya Kupigania Ukombozi wa Palestina, Hamas, imetangaza wazi kuwa haitakubali jaribio lolote la kuipokonya silaha, ikionya dhidi ya kuingiliwa mambo ya Palestina na mataifa ya kigeni. Hamas imesisitiza kuwa inahitaji dhamana zilizo wazi na madhubuti zaidi kwa awamu ya pili ya makubaliano ya kusitisha mapigano na utawala wa Israel.

Katika mahojiano na televisheni ya al-Masirah ya Yemen siku ya Jumanne, Osama Hamdan alisisitiza kuwa Hamas kamwe haitakabidhi silaha zake kwa nguvu za kigeni. Amesema: “Hamas inapinga kuwasili kwa majeshi ya kigeni ili kutupokonya silaha ambazo utawala vamizi wa Israel umeshindwa kuzichukua… Wazo la kusalimisha silaha ni jambo ambalo Muqawama haitalikubali.”

Hamdan pia alizungumzia makubaliano ya kusitisha mapigano na Israel, ambayo alisema yameendelea kukiukwa na utawala huo, akisisitiza haja ya dhamana zilizo wazi zaidi katika hatua inayofuata.

Alionya kuwa kuendelea kwa mzingiro wa Gaza ni dalili ya kurejea kwa uhasama. Amesema: “Kushindwa kufungua mipaka ni ishara kwamba adui anakusudia kurejea katika mashambulizi dhidi ya Ukanda wa Gaza.”

Aidha, alibainisha kuwa kutumia mzingiro kama silaha hakutavunja mapambano ya Wapalestina, akisema kutumia vizuizi vya misaada ya kimsingi kama chombo cha vita “kunazidisha chuki dhidi ya taasisi ya Kizayuni.”

Akilaani sera za Israel na Marekani katika eneo, Hamdan amesema kuwa sera hizo ni sehemu ya mkakati mpana wa kijeshi wa kutaka kutawala Asia ya Magharibi.

Licha ya mashambulizi yanayoendelea dhidi ya Wapalestina, Hamdan amesema ana imani katika ustahimilivu wa Wapalestina.

Makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyosimamiwa na Marekani kati ya Hamas na Israel yalifikiwa Oktoba 10, 2025. Katika awamu ya kwanza, Israel ilitakiwa kufungua mipaka yote ya Gaza, kuruhusu chakula na misaada kuingia na kumaliza uhasama kwa kubadilishana na kuachiliwa kwa mateka wote waliokuwa mikononi mwa Hamas.

Ingawa Hamas imefuata makubaliano hayo, Israel imeendelea kushambulia Gaza na kufunga mipaka mingi, ikizuia misaada muhimu.

Tangu kusitishwa kwa mapigano kuanza, Israel imeua Wapalestina wasiopungua 411 huko Gaza na kujeruhi wengine 1,112.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Gaza, jumla ya waliouawa Gaza tangu Oktoba 2023, wakati Israel ilipoanzisha vita vya mauaji ya kimbari, imefikia watu 70,937, huku angalau 171,192 wakiwa wamejeruhiwa.

 

 

 

 

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *