Bunge la Algeria jana Jumatano lilipasisha kwa kauli moja sheria inayotambua ukoloni wa Ufaransa nchini humo kuwa no jinai, ikiutaja kuwa ni “uhalifu wa serikali,” na kuitaka Ufaransa iombe msamaha rasmi kwa jinai hiyo.

Wawakilishi wa watu wa Algeria walisimama chini ya kuba la Bunge la Taifa wakiwa wamevaa shali zenye rangi za bendera ya Algeria, na kupiga makofi kwa muda mrefu baada ya kupitishwa sheria hiyo ambayo inaitwisha serikali ya Ufaransa “dhima ya kisheria kwa historia yake ya ukoloni nchini Algeria na maafa iliyoyasababisha.”

Sheria hiyo imeorodhesha “uhalifu wa ukoloni wa Ufaransa,” ikiwa ni pamoja na “mauaji nje ya mfumo wa mahakama, mateso, ubakaji, majaribio ya silaha za nyuklia katika ardhi ya Algeria na uporaji wa utajiri wa kimfumo.”

Wakati wa kuwasilishwa rasimu ya sheria hiyo bungeni siku chache zilizopita, Ibrahim Boughali Spika wa Bunge la Algeria alisema ni wakati makhsusi kwa Algeria ya leo ambapo serikali, kupitia chombo chake cha kutunga sheria, inahuisha jukumu lake kwa kumbukumbu ya kitaifa na dhamiri ya historia.

Spika wa Bunge la Algeria aliongeza kusema: Mradi wa kikoloni wa Ufaransa haukuishia kwenye uporaji wa mali tu, bali pia ulienea hadi kwenye sera za kimfumo za kusababisha umaskini, njaa na kutengwa watu kwa lengo la kuharibu upendo wa Waalgeria, kufuta utambulisho wao na kukata uhusiano na mizizi yao ya kihistoria na kitamaduni.

Kuidhinishwa sheria hiyo kunakuja wakati Paris na Algiers zikiwa katika mgogoro mkubwa wa kidiplomasia.

Sheria ya kutambua ukoloni wa Ufaransa nchini Algeria kuwa ni uhalifu inasisitiza kwamba “fidia kamili na ya usawa kwa uharibifu wote wa kimwili na kimaadili unaosababishwa na ukoloni wa Ufaransa ni haki thabiti ya serikali na watu wa Algeria.”

Sheria hiyo inailazimisha serikali kuitaka Ufaransa “kutambua na kuomba msamaha rasmi kwa historia yake ya ukoloni” na “kusafisha maeneo ya majaribio yake ya silaha za nyuklia” ndani ya Algeria.

Rais Abdelmajid Tebboune wa Algeria aliwahi kukosoa na kulaani jinai zilizofanywa na Ufaransa huko Algeria na kueleza kuwa, ukoloni wa Ufaransa nchini kwake kuanzia mwaka 1830 hadi 1962 ulifanya uhalifu wa kutisha sana ambao haujashuhudiwa katika historia ya sasa ya mwanaadamu.

Zaidi ya Waalgeria milioni moja waliuawa katika mapambano ya ukombozi ya kuwafukuza wakoloni wa Kifaransa nchini humo. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *