
Kutoka Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro, kiongozi wa kanisa Katoliki duniani, Papa Leo XIV, ameongoza sherehe ya Ekaristi ya kuadhimisha kuzaliwa kwa Kristo. Krismasi hii inaambatana na mwisho wa Mwaka wa Jubilei, iliyozinduliwa mwaka mmoja uliopita na Papa Francis.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Na mwandishi wetu huko Roma, Éric Sénanque
Kwa Misa hii ya kwanza ya Krismasi huko Vatican wakati wa Upapa wa Leo XIV, waumini 6,000 walikuwa wameketi katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro. Wengine 5,000 walivumilia mvua katika uwanja wa nje, na Papa Leo XIV amehakikisha anawasalimia kabla ya sherehe.
Ujumbe wa Krismasi “si suluhisho la matatizo yote,” Papa amesema katika mahubiri yake, “bali ni hadithi ya upendo inayotuhusisha sote dhii ya vurugu na ukandamizaji. Mungu huwasha mwanga mpole unaoangazia wokovu wa watoto wote wa ulimwengu huu.”
Hotuba ya kiroho sana, lakini pia yenye misingi ya kisiasa: “Ingawa uchumi uliopotoka unasababisha kuwatendea watu kama bidhaa,” amesikitika Leo XIV, “Mungu anajifananisha na sisi, akifunua heshima isiyo na kikomo ya kila mtu.”
Papa pia amekumbusha kwamba mwaka mmoja mapema, mtangulizi wake, Francis, alizindua, katika kanisa hilo, Jubilei ya Matumaini, ambayo sasa inakaribia kukamilika. Mwaka huu Mtakatifu umewaleta karibu mahujaji milioni 30 Roma. Krismasi ni sikukuu ya imani, upendo, na matumaini, mkuu wa Kanisa Katoliki pia amebainisha. Leo Alhamisi, Desemba 25 saa sita mchana, Siku ya Krismasi, Papa atatoa baraka yake ya “Urbi et Orbi”, kwa jiji na ulimwengu, katika matangazo ya kimataifa, na anatarajiwa kuorodhesha migogoro mbalimbali inayoivunja dunia ili kuwasilisha ujumbe wa amani.